49. Kuharakisha kulipa deni la Ramadhaan kabla ya kuingia Ramadhaan nyingine

Tambueni ya kwamba anayefungua katika Ramadhaan kwa sababu iliyoruhusiwa, kama nyuduru zinazokubalika katika Shari´ah zinazomruhusu kufungua, au kwa sababu iliyo haramu, kama yule aliyevunjilia swawm yake kwa jimaa au kwa jambo jingine, basi ni wajibu juu yake kulipa. Amesema (Ta´ala):

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“… basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo.”[1]

Inapendekezwa kwake aharakishe kulipa ili kuondoa deni lililo juu ya dhamira yake. Aidha inapendekezwa ulipaji uwe kwa mfululizo, kwa sababu ulipaji hufanana na utekelezaji wa awali. Ikiwa hakulipa mara moja, ni wajibu awe na azma ya kulipa.

Inajuzu kwake kuchelewesha kwa sababu wakati wake umewekwa mpana. Kila wajibu wenye wakati mpana unaruhusiwa kuuchelewesha pamoja na azma ya kuutekeleza. Pia inaruhusiwa kuutenganisha kwa kufunga siku zilizotawanyika. Lakini ikiwa haijabaki katika Sha´baan isipokuwa kiasi cha siku anazodaiwa, basi ni wajibu juu yake kufunga kwa mfululizo kwa maafikiano ya wanazuoni kutokana na kubana kwa wakati na katika hali hiyo haifai kuchelewesha mpaka baada ya Ramadhaan nyingine bila udhuru. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

”Ilikuwa inanibaki juu yangu swawm ya Ramadhaan, nami sikuweza kuilipa isipokuwa katika Sha´baan kwa sababu ya nafasi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Hili linafahamisha kwamba wakati wa kulipa ni mpana mpaka pale panapobaki katika Sha´baan siku zilizo sawa na anazodaiwa, basi hapo ni wajibu juu yake kuzifunga kabla ya kuingia Ramadhaan mpya. Akichelewesha ulipaji mpaka ikamkuta Ramadhaan mpya, basi atafunga Ramadhaan ya sasa, kisha atalipa baada yake. Kisha ikiwa kuchelewesha kwake kulitokana na udhuru ambao haukumwezesha kulipa katika kipindi hicho, basi hana juu yake chochote isipokuwa kulipa. Ikiwa ilikuwa bila udhuru, basi ni wajibu juu yake pamoja na kulipa, kumlisha chakula masikini mmoja kwa kila siku nusu pishi ya chakula cha watu wa eneo lake.

[1] 02:183-184

[2] al-Bukhaariy (1950) na Muslim (1146).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 46
  • Imechapishwa: 19/03/2026