48. Maoni ya Ibn Taymiyyah kuhusu kupangusa juu ya soksi

7 – Maoni ya Ibn Taymiyyah:

Amesema (Rahimahu Allaah):

”Inajuzu kupangusa juu ya soksi ikiwa mtu anatembea nazo, ni mamoja ziwe za ngozi au zisiwe za ngozi. Haya ndio maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Imepokelewa kwamba:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha na akapaka juu ya soksi na viatu.”

Hadiyth hii, ikiwa haikuthibiti, basi kipimo kinaithibitisha. Kwa sababu tofauti kati ya soksi na viatu ni kwamba hii ni ya sufu na hii ni ya ngozi. Inajulikana kwamba tofauti kama hii haina athari katika Shari´ah. Kwa hiyo hakuna tofauti soksi iwe ni ngozi, pamba, kitani au sufu, kama ambavyo hakutofautisha kati ya weusi wa vazi katika Ihraam na weupe wake. Kikubwa kinachoweza kusemwa ni kwamba ngozi hudumu zaidi kuliko sufu. Kitu kama hicho hakina athari, kama vile haina athari kwamba ngozi ni imara. Bali inajuzu kupaka juu ya kinachodumu na kisichodumu.

Vilevile inajulikana kwamba haja ya kupaka juu ya hiki ni kama haja ya kupaka juu ya kile. Ikiwa hekima na haja vinalingana, basi kutofautisha kati ya hivyo viwili ni kutofautisha kati vitu viwili vinavyolingana, jambo ambalo ni kwenda kinyume cha uadilifu na kipimo sahihi kilichokuja nayo Qur-aan, Sunnah, yale ambayo Allaah ameyateremsha ndani ya vitabu Vyake na kuwatuma kwayo Mitume wake. Yule mwenye kutofautisha kwa kusema hii inapenyeza maji na hii haipenyezi, ametaja tofauti ya kimaumbile isiyo na athari. Lau angesema msemaji kwamba maji hufika kwenye sufu zaidi kuliko ngozi, basi kupangusa juu yake kunakuwa na kipaumbele zaidi kwa kushikamana kwa twahara juu yake zaidi, basi sifa hii ingekuwa na uzito zaidi katika kuzingatiwa kuliko ile sifa na ingekuwa karibu zaidi na sifa zenye athari; na ile iko karibu zaidi na sifa zisizo na athari, ingawa zote mbili ni batili.

Vilevile mashimo ya kuchanika hayazuii kujuzu kupangusa. Inafaa kupangusa juu ya soksi hata kama zinahitaji kufungwa. Haya ndio maoni sahihi. Vivyo hivyo buti ndefu ambayo inahitaji kufungwa ili ikae imara na kufunika – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.”[1]

Amesema (Rahimahu Allaah) katika fatwa nyingine:

”Inajuzu kupaka juu ya buti inayofunika vifundo viwili ikiwa inasimama na kubaki yenyewe bila kamba. Ikiwa haisimami na haibaki isipokuwa kwa vifungo au mikanda, pia inajuzu kupaka juu yake. Kwa sababu inasitiri mahali pa faradhi yenyewe. Vivyo hivyo soksi ambayo haisimami na kubaki isipokuwa kwa nyuzi. Na lau ilisimama na kubaki kwa kitu kilicho nje yake kama soksi isiyosimama isipokuwa kwa kiatu, basi inajuzu kupaka juu yake, ni mamoja iwe ni ya sufu ngumu, sufu laini, pamba, kitani au ngozi. Hakuna haja ya kuzingatia masharti yasiyo na asili katika Shari´ah na yanayorudisha lengo la ruhusa kwa kulibatilisha.”

Amesema pia katika fatwa nyingine:

”Inajuzu kupaka juu ya vitambaa vinavyofungwa mguuni[2], navyo ni kwamba mtu afunge mguuni vitambaa kwa sababu ya baridi, kwa kuogopa kutembea peku, kwa sababu ya majeraha yaliyopo mguuni na mfano wa hayo. Kupaka juu yake kunastahiki zaidi kuliko kupaka juu ya soksi za ngozi na soksi za kawiada. Kwa sababu vitambaa hivyo hutumika kwa haja katika ada na kuvivua kuna madhara, ima kupata baridi, kuumia kwa kutembea peku au kuathirika kwa jeraha. Kwa hiyo ikiwa imejuzu kupaka juu ya soksi za ngozi na soksi za kawaida, basi kupangusa juu ya vitambaa kuna haki zaidi ya kufaa.”

Amesema tena:

”Ni jambo linalotambulika kwamba katika nchi za baridi kuna haja ya kupangusa juu ya vitambaa vya joto na juu ya vilemba, jambo ambalo halihitajiki katika ardhi ya Hijaaz. Basi watu wa Shaam, Ruum na mfano wa nchi hizo wana haki zaidi ya ruhusa hii kuliko watu wa Hijaaz… Wakikatazwa kupaka juu yake, basi watakuwa wameleta dhiki inayoonekana kuwa kinyume na Shari´ah bila hoja yoyote kabisa waliyonayo.”

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (21/214-215).

[2] Vitambaa (bendeji) hizo vinaingia katika ujumla wa Hadiyth ya Thawbaan iliyotajwa hapo awali, ambapo Mtume (amani na baraka ziwe juu yake) aliwaamuru wapanguse juu ya vitambaa vya kufunika miguu. (al-Qaasimiy)

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 71-74
  • Imechapishwa: 21/04/2026