43- Ni lazima kulibeba jeneza na kulisindikiza. Kufanya hivo ni haki ya muislamu juu ya muislamu mwenzake. Kuhusu hayo zimepokelewa Hadiyth. Nitataja mbili katika hizo:

Ya kwanza: Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Haki ya muislamu [Katika upokezi mwingine imekuja: “Inamlazimu muislamu juu ya nduguye] mambo matano: “Kuitikia salamu, kumtembelea mgonjwa, kulisindikiza jeneza, kuitikia mwaliko na kumtakia rehema mwenye kuchemua.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/88) na mtiririko ni wake, Muslim (07/03) kwa upokezi wa pili, Ibn Maajah (01/439), Ibn-ul-Jaaruud (261), Ahmad (02/372, 412, 540). Katika upokezi wake mwingine amesema:

“… ni sita.”

Akazidisha:

“Akikuomba ushauri basi mshauri.”

Ni upokezi wa Muslim pia. Wote wameipokea kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah.

Kuhusiana na maudhui haya ipo Hadiyth kutoka kwa al-Baraa´ bin ´Aaziyb iliopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim na wengineo.

Ya pili: “Watembeleeni wagonjwa na yasindikizeni majeneza yatakukumbusheni Aakhirah.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” (04/73), al-Bukhaariy katika “al-Adab al-Mufrad”, uk. 75, Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (709- al-Mawaarid), at-Twayaalisiy (01/224) na Ahmad (03/27, 32, 48), al-Baghawiy katika “Sharh-us-Sunnah” (01/166/01) kutoka katika Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy.

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

Hadiyth hiyo ina ushahidi mwingine kutoka kwa ´Awf bin Maalik bila ya kipande cha mwisho. Ameipokea at-Twabaraaniy. Rejea katika “al-Majmaa´” (02/299).

44- Kulisindikiza jeneza kuna ngazi mbili:

Ya kwanza: Kulisindikiza kuanzia kwa familia yake mpaka mtu akamswalia.

Ya pili: Kulisindikiza kuanzia kwa familia yake mpaka akamaliza kuzikwa.

Yote mawili yamefanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia akisema:

“Tulikuwa tukimtangulia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) (bi maana al-Madiynah) pindi anapohudhurishwa kwetu maiti kisha tunamjuza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akaja na akamuombea msamaha mpaka pale itapofishwa ndipo huondoka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale waliokuwa pamoja naye mpaka azikwe. Wakati mwingine hurefuka kuzuilika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati tulipochelea jambo la kumtilia uzito ndipo wakasema baadhi ya watu kuwaambia wengine: “Lau tungelikuwa hatumjuzi Mtume chochote mpaka pale anapofishwa. Anapofishwa ndipo tumjuze. Kufanya hivo hakutokuwa na kumtilia uzito wala kuizilika. Tukafanya hivo na tulikuwa tukimjuza kuhusu maiti baada ya yeye kufa. Baada ya hapo ndipo anakuja na kumswalia. Mara huondoka na mara nyingine hubakia mpaka maiti azikwe. Tulifanya hivo kwa kipindi fulani. Kisha tukaambizana: “Lau Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingekuja kwa nafsi yake na tukayabebea majeneza yetu kumpelekea yeye ili amswalie nyumbani kwake basi jambo hilo lingelikuwa ni bora na rahisi kwake. Tukafanya hivo na hali iliendelea hivo mpaka hii leo.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (753- Mawrid), al-Haakim (01/353-364-365), al-Bayhaqiy amepokea kutoka kwake (03/74), Ahmad (03/66) Hadiyth mfano wake. al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

Ni Swahiyh peke yake. Kwa sababu ndani yake yumo Sa´iyd bin ´Ubayd bin Sibaaq na hakutolewa chochote.

45- Hapana shaka kwamba ngazi ya pili ni bora kuliko ngazi ya kwanza kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kuhudhuria jeneza [kuanzia nyumbani kwake] [Katika upokezi mwingine: “Yule atakayesindikiza jeneza la muislamu hali ya kuwa na imani na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah] mpaka akaswaliwa, basi anapata Qiraatw na yule mwenye kulidhuhuria mpaka akazikwa [katika upokezi mwingine:  “Mpaka wakamaliza] basi ana al-Qiraatw mbili [ya ujira]. Kukasemwa: [“Ee Mtume wa Allaah!] al-Qiraatw mbili ni kitu gani?” Akasema: “Ni mfano wa milima miwili mikubwa.” [Katika upokezi mwingine imekuja: “Kila al-Qiraatw ni mfano wa Uhud.]

Ameipokea al-Bukhaariy (01/89-90, 03/150-151), Muslim (03/51-52), Abu Daawuud (02/63-64), an-Nasaa´iy (01/282), at-Tirmidhiy (02/150) ambaye ameisahihisha, Ibn Maajah (01/467-468), Ibn-ul-Jaaruud (261), al-Bayhaqiy (03/412-413), at-Twayaalisiy (2581), Ahmad (02/233, 246, 320, 401, 458, 470, 474, 493, 521, 531) kupitia njia nyingi kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

Upokezi wa pili ni wa al-Bukhaariyu, an-Nasaa´iy na Ahmad.

Ziada ya kwanza ni ya Muslim, Abu Daawuud na wengineo. Ziada mbili za mwisho ni za an-Nasaa´iy. Hadiyth ina shawahidi zengine kutoka kwa japo la Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

Katika upokezi wa an-Nasaa´iy imekuja:

“… kuliko Uhud.”

Hadiyth hii ina Hadiyth nyingine yenye kuitolea ushahidi kwa Ubayd bin Ka´b kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa tamko lisemalo:

“… nzito zaidi kwenye mizani yake kuliko Uhud.”

Ameipokea Ahmad (05/131), Ibn Maajah (01/468) kwa tamko la an-Nasaa´iy. Nayo ni nzuri. Ziada ya kwanza ni ya Muslim, Abu Daawuud na isiyokuwa hiyo. Ziada mbili zengine ni za an-Nasaa´iy. Hadiyth ina shawahidi zengine kutoka kwa japo la Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

Ya kwanza: Kutoka kwa Thawbaan kwa Muslim na at-Twayaalisiy (985), Ahmad (05/276-277, 282-283-284).

Ya pili na ya tatu: Kutoka kwa al-Baraa´ bin ´Aazib na ´Abdullaah bin Mughaffal kwa an-Nasaa´iy na Ahmad (04/86, 294).

Ya nne: Kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy. Ameipokea Ahmad (03/20, 27, 97) kupitia njia mbili kutoka kwake. Hadiyh hii ina shawahidi zengine ambazo zimetajwa na al-Haafidhw katika “al-Fath” (03/153).

Katika baadhi ya shawahidi kupitia kwa Abu Hurayrah kuna ziada zenye manufaa ambazo pengine ni vyema kuzitaja:

“Ibn ´Umar alikuwa akimswalia kisha akiondoka zake. Wakati alipofikiliwa na Hadiyth ya Abu Hurayrah akasema: “Abu Hurayrah ametushinda.” [Katika upokezi mwingine imekuja: “Akalikuza jambo hilo.”] [Akamtuma Khabbaab kwenda kwa ´Aaishah amuulize kuhusiana na maneno ya Abu Hurayrah kisha arejee kwake kumweleze aliyoyasema. Kipindi hicho Ibn ´Umar akachota kwa mkono wake rundo la vijiwe vya msikitini akivigeuzageuza mkononi mwake mpaka akamrejelea yule mjumbe ambapo akasema: “´Aaishah amesema: “Abu Hurayrah amesema kweli.” Ibn ´Umar akazipiga zile changarawe ardhini kisha akasema:] “Hakika tumepitwa na Qiraatw nyingi.” [Jambo hilo likamfikia Abu Hurayrah ambapo akasema: “Hakika si vyenginevyo sikuwa mimi nashughulishwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na jambo la biashara wala kilimo. Hakika si vyenginevyo nilikuwa ni mwenye kulazimiana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya neno atalonifundisha na kwa ajili ya tonge atalonilisha.] [Ibn ´Umar akamwambia: “Hakika wewe Abu Hurayrah ndiye ulikuwa ukilazimiana zaidi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliko sisi na mjuzi zaidi wa Hadiyth zake.”].

Ziada zote hizi ni za Muslim isipokuwa ya mwisho ambayo ni ya Ahmad (02/2-3, 387) na pia Sa´iyd bin Mansuur kwa cheni ya wapokezi ambayo ni Swahiyh, kama alivosema al-Haafidhww katika “al-Fath”. Ambayo iko kabla yake ni ya at-Twayaalisiy na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Ziada ya pili ni ya al-Bukhaariy na Muslim, upokezi wa pili juu yake ni wa at-Tirmidhiy na Ahmad.

Upokezi wa mwisho unasema wazi kwamba Ibn ´Umar aliwasiliana mwenyewe na Abu Hurayrah. Hayo yanatiliwa nguvu na upokezi wa Muslim na wengineo kwa tamko lisemalo: “Ibn ´Umar akasema: “Abu Hurayrah! Tazama kile unachohadithia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Abu Hurayrah akasimama mpaka wakaondoka kwenda kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambapo akamwambia: “Ee mama wa waumini! Nakuuliza kwa jina la Allaah, je, ulimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Akaitaja ile Hadiyth.” Akajibu: “Ee Allaah! Ndio.” Abu Hurayrah akasema: “Hakika si vyenginevyo sikuwa mimi… “

Udhahiri wa yote haya yana tofautiana kwamba alimwagiza Khabbaab kwa Ibn ´Umar.

al-Haafidhw Ibn Hajar ameoanisha kati ya mapokezi mawili kwamba mjumbe wakati aliporejea kwa Ibn ´Umar kumweleza aliyosema ´Aiashah khabari hizo zilimfikia Abu Hurayrah ambapo akaenda kwa Ibn ´Umar na akayasikia hayo kutoka kwenye mdmo wa ´Aaishah.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) anayo Hadiyth nyingine juu ya fadhilah za kuhudhuria jeneza. Amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni nani katika yenu aliyeamka leo hali ya kuwa amefunga?” Abu Bakr akajibu: “Mimi.” Akauliza tena: “Ni nani katika yenu ambaye hii leo amemtembelea mgonjwa?” Abu Bakr akajibu: “Mimi.” Akauliza tena: “Ni nani kati yenu ambaye hii leo ameshuhudia jeneza?” Abu Bakr akajibu: “Mimi.” Ni nani ambaye hii leo amemlisha maskini?” Abu Bakr akajibu: “Mimi.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Sifa hizi hazikusanyiki kwa mtu kwa siku moja isipokuwa ataingia Peponi.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake (03/92, 07/110), al-Bukhaariy katika “al-Adab al-Mufrad”, uk. 75.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 85-90
  • Imechapishwa: 06/07/2020