48. Kinga yako bora dhidi ya adhabu ya Allaah

Imaam Ahmad amesimulia kutoka kwa ´Abdul-´Aziyz bin Abiy Salamah al-Maajashuun, kutoka kwa Ziyaad bin Abiy Ziyaad, mtumwa wa ´Abdullaah bin ´Ayyaash bin Abiy Rabiy´ah, ambaye amemweleza kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna tendo ambalo mwanadamu amelifanya litakalomwokoa zaidi kutokana na adhabu ya Allaah kuliko kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).” Mu´aadh ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Je nikujulisheni matendo yenu bora kabisa, yaliyo safi zaidi mbele ya Mfalme wenu, yaliyo ya juu zaidi katika daraja zenu, bora zaidi kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha na bora zaidi kuliko kukutana na adui yenu mkiwapiga shingo zao nao wakiwapiga shingo zenu?” Wakasema: “Ndiyo, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ni kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).”[1]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hawakai watu kutoka katika kikao pasi na kumtaja Allaah (Ta´ala) ndani yake, isipokuwa wataondoka kama maiti ya punda na watakuwa na majuto juu yao.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud.

Imekuja kwa at-Tirmidhiy:

“Hawaketi watu katika kikao chochote pasi na kumtaja Allaah ndani yake na wala wasimswalie Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), isipokuwa kitakuwa ni majuto dhidi yao; Akitaka atawaadhibu, na akitaka atawasamehe.”[3]

Abu Muslim al-Agharr amesema: Nashuhudia ya kwamba Abu Hurayrah na Abu Sa´iyd wametoa ushuhuda kuwa wamemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hawakai watu katika kikao wakimtaja Allaah (´Azza wa Jall) ndani yake isipokuwa huwazunguka Malaika, huwafunika rehema, huwashukia utulivu na Allaah huwataja kwa wale walioko Kwake.”[4]

Ameipokea Muslim.

´Abdullaah bin Busr ametaja kwamba bwana mmoja alisema:

”Ee Mtume wa Allaah! Milango ya kheri ni mingi na siwezi kufanya yote. Hivyo basi nijulishe unachotaka nikishikilie na usinizidishie nikasahau.” Akamjibu: ”Ulimi wako usiache kuwa na unyevu kwa kumtaja Allaah.”[5]

[1] Ahmad (7/367-368). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1493).

[2] Ahmad (3/422) na Abu Daawuud (4821). Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim, adh-Dhahabiy na al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (179).

[3] Ahmad (3/573) na at-Tirmidhiy (3380), aliyesema kuwa ni nzuri na Swahiyh. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (73-78).

[4] Muslim (2700).

[5] Ahmad (17227), at-Tirmidhiy (3375), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri, na Ibn Maajah (3793). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (3).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 83-86
  • Imechapishwa: 17/08/2025