Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

مَلِكِ يَوْمِ الدِّينِ

”Mfalme wa siku ya Malipo!”[1]

Ni siku ya malipo na hesabu. Siku ambayo kila mmoja atalipwa kwa matendo yake. Kama ni mema malipo yatakuwa mema, na kama ni shari malipo yatakuwa shari. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”Ni kipi kitakachokujulisha siku ya malipo? Kisha nini kitakachokujulisha siku ya malipo? Siku ambayo nafsi haitomiliki chochote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”[2]

Hadiyth kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye akili ni yule ambaye anaibidisha nafsi yake na kufanyia kazi kwa yanayomgonja baada ya mauti na asiye muweza ni yule ambaye anafuata matamanio ya nafsi yake na huku akiwa na matumaini ya uongo kwa Allaah.”[3]

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Mmiliki wa kila kitu. Yeye ni Mmiliki wa ulimwengu na Aakhirah. Kutajwa maalum siku ya Malipo hapa kwamba Allaah ndiye Mmiliki wake ni kwa sababu hiyo ni siku ambayo viumbe wote watanyenyekea kwa Mola wa walimwengu. Hili ni kinyume na ulimwenguni, ambapo waliwahi kuwepo walioasi na kujikweza na wakasema:

أنا ربكم الأعلى

“Mimi ndiye Mola wenu mkuu.”[4]

مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي

“Sijui kama mnaye mungu badala yangu.”[5]

Hadiyth aliyotaja Shaykh ameipokea at-Tirmidhiy (2459). Hata hivyo katika cheni yake ya wapokezi yupo Abu Bakr bin Abiy Maryam ambaye ni dhaifu.

[1] 01:03

[2] 82:17-19

[3] at-Tirmidhiy (2459) aliyesema ni nzuri, Ibn Maajah (4260) na Ahmad (17123). at-Tirmdhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri.”

al-Haakim  amesema:

”Hadiyth hii ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti ya al-Bukhaariy japo hakuipokea.” (al-Mustadrak (01/125)).

[4] 79:24

[5] 28:38

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 04/06/2026