47. Maana ya kila mtoto huzaliwa juu ya Fitwrah

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا

“Basi [wewe mwenye kutafuta haki] uelekeze uso wako wote kwenye imani iliyosafi na ya asli, imani ambayo Allaah [wakati wa uumbaji] amewaumbia watu kwayo.” 30:30

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mtoto yeyote isipokuwa huzaliwa juu ya Fitwrah.”

Wanachuoni wametofautiana ni nini maana ya Fitwrah.

Maoni ya kwanza yanasema kuwa Fitwrah ni Uislamu. Haya yamesemwa na Abu Hurayrah, Ibn Shihaab na wengine na ni moja katika maoni ya Imaam Ahmad. Pindi ´Abdil-Barr alipotaja tofauti hizi katika kitabu chake “at-Tamhiyd” alisema:

“Wengine wanasema kuwa Fitwrah hapa maana yake ni Uislamu. Haya ndio maoni yanayojulikana kwa Salaf wengi na wafasiri wa Qur-aan… Kuhusu maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا

“Basi [wewe mwenye kutafuta haki] uelekeze uso wako wote kwenye imani iliyosafi na ya asli, imani ambayo Allaah [wakati wa uumbaji] amewaumbia watu kwayo.” 30:30

wameafikiana ya kwamba maana yake ni Uislamu.

Hata hivyo sivyo. al-Qurtwubiy na wafasiri wengine wa Qur-aan wametaja tafsiri nyingi juu ya Aayah. al-Qurtwubiy amesema:

“Kuna tafsiri nyingi juu ya neno Fitwrah. Moja wapo ni Uislamu. Maoni haya ndio yenye kujulikana kwa Salaf wengi… Kujengea juu ya hili mtoto ni mwenye kuzaliwa hali ya kuwa amesalimika kutokamana na ukafiri na juu ya fungamano alilochukua Allaah kutoka katika dhuriya ya Aadam alipowatoa kutoka kwenye uti wake wa mgongo. Kwa hiyo mtoto akifa kabla ya kubaleghe anaingia Peponi pasi na kujali ni mtoto wa waislamu au wa makafiri.

Maoni ya pili yanasema kuwa Fitwrah ni ule msingi ambao Allaah amemuumba mwanaadamu nao kuanzia kwamba amewaumba katika uhai, kifo, furaha na kutokuwa na furaha.

Maoni ya tatu yanasema Fitwrah haiwahusu watu wote na kwamba inawahusu waumini peke yao. Kwa kuwa lau angeliwaumba wote juu ya Uislamu asingelifuru yeyote.

Maoni ya tatu yanasema kuwa Fitwrah ni uumbaji ambao mtoto mchanga anaumbwa kwao kumtambua Mola wake. Ni kana kwamba kila mtoto mchanga anaumbwa kwa uumbaji anaomtambua Mola wake pindi anapofikia kiwango hicho cha utambuzi. Wale wenye maoni haya wamestadili kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَا لِيَ لَا أَعْبُدُ الَّذِي فَطَرَنِي وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

“Kwa nini mimi nisimwabudu Ambaye ameniumba? Kwake [hatimaye ndiko] mtarejeshwa.” 36:22

Kinacholengwa ni kwamba watoto wanakufa juu ya Tawhiyd na Uislamu ambao Allaah amewaumba kwavyo. Ni katika watu wenye furaha wa Aakhirah ambao wanastahiki kuingia Peponi bila ya matendo yoyote waliyofanya na kutanguliza. Inahusiana na huruma na upole wa Allaah kwao:

ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ

“Hiyo ni fadhila ya Allaah humtunuku yule amtakaye – na Allaah ni Mwenye fadhila kubwa.” 57:21

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 99-101
  • Marejeo: Firqatunnajia.com
  • Imechapishwa: 16/10/2016