129 – Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwa kusema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitufundisha Istikhaarah katika mambo yote kama vile anavyotufunza Suurah ndani ya Qur-aan. Akisema: ”Mmoja wenu akikusudia kufanya jambo, basi aswali Rak´ah mbili zisizo za faradhi, kisha aseme:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْتَخِيرُكَ بِعِلْمِكَ، وَأَسْتَقْدِرُكَ بِقُدْرَتِكَ، وَأَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ العَظِيمِ، فَإِنَّكَ تَقْدِرُ وَلاَ أَقْدِرُ، وَتَعْلَمُ وَلاَ أَعْلَمُ، وَأَنْتَ عَلَّامُ الغُيُوبِ، اللَّهُمَّ إِنْ كُنْتَ تَعْلَمُ أَنَّ هَذَا الأَمْرَ خَيْرٌ لِي فِي دِينِي وَمَعَاشِي وَعَاقِبَةِ أَمْرِي – أَوْ قَالَ: عَاجِلِ أَمْرِي وَآجِلِهِ – فَاقْدُرْهُ لِي، وَيَسِّرْهُ لِي، ثُمَّ بَارِكْ لِي فِيهِ، وَإِنْ كُنْتَ تَعْلَمُ أَنَّ هَذَا الأَمْرَ شَرٌّ لِي فِي دِينِي وَمَعَاشِي وَعَاقِبَةِ أَمْرِي – أَوْ قَالَ عَاجِلِ وَآجِلِهِ – فَاصْرِفْهُ عَنِّي، وَاصْرِفْنِي عَنْهُ، وَاقْدُرْ لِي الخَيْرَ حَيْثُ كَانَ، ثُمَّ أَرْضِنِي به

”Ee Allaah! Hakika mimi nakutaka ushauri kwa ujuzi Wako na nakuomba uniwezeshe kwa uwezo Wako na nakuomba kutokana na fadhilah Zako tukufu. Hakika Wewe unaweza, nami siwezi, unajua, nami sijui Nawe ni mjuzi wa yaliyofichikana. Ee Allaah! Iwapo unajua kuwa jambo hili lina kheri nami katika dini yangu, maisha yangu na mwisho wa jambo langu” – au alisema: ”Duniani na Aakhirah” – basi nakuomba uniwezeshe nilipate na unifanyie wepesi kisha unibarikie kwacho. Endapo unajua kwamba jambo hili ni shari kwangu katika dini yangu, maisha yangu na mwisho wa jambo langu, basi liweke mbali nami, uniepushe nalo na nipangie jambo jengine lenye kheri nami popote lilipo, halafu niridhishe kwalo” au ataja haja yake.”[1]

MAELEZO

Isitikhaarah ni kumuomba Allaah akuwafikishe katika kheri kati ya mambo mawili. Istikhaarah inakuwa katika yale ambayo hayajabainika manufaa yake na yale ambayo haitambulika mwisho wake utakuweje, kama vile kumuoa mwanamke fulani, biashara, safari na mengineyo. Kuhusu yale ambayo manufaa au faida yake iko wazi hakuna kufanya Istikhaarah. Vivyo hivyo yale ambayo hukumu yake inatambulika kwa mujibu wa Shari´ah, kama vile swalah, hajj na kutoa zakaah, hakuna kufanya Istikhaarah labda ikiwa kwa mfano njia ya kwenda hajj ni yenye kutisha.

[1] al-Bukhaariy (1162).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 10/11/2025