Ukarimu una aina mbili:

1 – Ya juu kabisa ni kuwa mkarimu kwa kutoitamani mali ya watu wengine.

2 – Ni kutoa kile kilicho mikononi mwako.

Huenda mtu akawa ni miongoni mwa watu wakarimu zaidi hali ya kuwa hawapi watu kitu, kwa sababu amekuwa mkarimu kwa kutoitamani kilicho mikononi mwao. Hii ndio maana ya maneno ya baadhi ya watu:

“Ukarimu ni kuwa mtoaji wa mali yako na kuwa mwangalifu kuhusu mali ya wengine.”

Nimemsikia Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah – Allaah aitakase roho yake – akisema:

“Allaah (Ta´ala) alimfunulia wahy Ibraahiym na kumwambia: ”Je, unajua kwa nini nimekufanya kuwa kipenzi changu wa hali ya juu?” Akasema: ”Hapana.” Akaambiwa: ”Kwa sababu nimekuona kuwa unapenda kutoa zaidi kuliko kupokea.”

Hii ni sifa miongoni mwa sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye hutoa wala hapokei, hulisha wala halishwi. Naye ni Mkarimu zaidi ya wakarimu wote na Mtukufu zaidi ya watukufu wote. Viumbe wanaopendeza zaidi Kwake ni wale wanaojipamba kwa sifa zinazolingana na za Yeye, Yeye ni Mkarimu na anawapenda wakarimu miongoni mwa waja Wake, ni Mjuzi ambaye anawapenda wanazuoni, ni Muweza ambaye anawapenda mashujaa, ni Mzuri ambaye anapenda uzuri. at-Tirmidhiy amesema katika “al-Jaamiy´” yake: Muhammad bin Bashshaar ametuhadithia: Abu ´Aamir ametuhadithia: Khaalid bin Ilyaas ametukhabarisha, kutoka kwa Swaalih bin Abiy Hassaan: Nimemsikia Sa´iyd bin al-Musayyab akisema:

”Hakika Allaah ni mzuri na anapenda uzuri, ni msafi na anapenda usafi, ni mkarimu na anapenda ukarimu na ni mtoaji na anapenda utoaji. Safisheni vibanda vyenu wala msijifananishe na mayahudi.”

Nikamtajia al-Muhaajir bin Mismaar, ambaye akasema: ´Aamir bin Sa´d amenihadithia, kutoka kwa baba yake (Radhiya Allaahu ´anh), kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), isipokuwa kwamba yeye amesema:

”Safisheni uwanja wenu wa mbele.”[1]

Haya ni Hadiyth ngeni. Khaalid bin Ilyaas ni dhaifu.

at-Tirmidhiy amesema vilevile katika “al-Jaamiy´” yake: al-Hasan bin ´Arafah ametuhadithia: Sa´iyd bin Muhammad al-Warraaq ametuhadithia, kutoka kwa Yahyaa bin Sa´iyd, kutoka kwa al-A´raj, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Mtu mkarimu yuko karibu na Allaah, karibu na Pepo, karibu na watu na mbali na Moto. Mtu mbakhili yuko mbali na Allaah, mbali na Pepo, mbali na watu na karibu na Moto. Mjinga mkarimu ni mpendwa zaidi kwa Allaah kuliko mfanya ´ibaadah mbakhili.”[2]

[1] at-Tirmidiy (2799). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2799).

[2] at-Tirmidhiy (1961), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni ngeni. Dhaifu mno kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (1961).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 76-79
  • Imechapishwa: 13/08/2025