42. Asiyejisalimisha kwa Tawhiyd ni mwenye kiburi na mkaidi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msomee aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake na kuyaweka wazi.

MAELEZO

Bi maana msomee Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah aliyoitaja Allaah (Ta´ala) ndani ya Qur-aan. Ameanza (´Azza wa Jall) kwayo. Halafu ameianza na kuikariri ili iweze kukita kwenye mioyo ya watu na ili hoja iweze kuwasimamia. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Na Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi Niabuduni.” (21:25)

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah, na Malaika, na wenye elimu wameshuhudia kwamba hakika hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana muabudiwa wa haki ila Yeye Mwenye nguvu Aliyeshinda, Mwenye hekima.” (03:18)

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Na Mungu wenu ni Mmoja pekee; hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.” (02:163)

يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ

“Enyi waja Wangu ambao mmeamini! Hakika ardhi Yangu ni pana, basi Mimi pekee Niabuduni.” (29:56)

Kuna Aayah nyingi mfano wake zenye kuwajibisha kumuabudu Allaah (´Azza wa Jall) peke Yake na si mwengine. Akikinaika na hilo, basi lengo limefikiwa. Asipofanya hivo, huyo ni mwenye kiburi na ni mkaidi. Kwa hivyo atakuwa ni mwenye kuingia katika maneno Yake (Ta´ala):

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ

“Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha kwa dhuluma na majivuno. Basi tazama vipi ilikuwa mwisho wa mafisadi.” (27:14)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 60-61
  • Imechapishwa: 11/11/2023