123 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mafukara walikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Matajiri wameondoka wakiwa na ngazi za juu na starehe za kudumu kutokana na mali zao na; wanaswali kama tunavyoswali na wanafunga kama tunavyofunga. Aidha wanayo nafasi ya mali ambayo wanahiji kwayo, kufanya ´Umrah, wanapambana jihaad na wanatoa swadaqah.”Hivi nisikuelezeni yale ambayo mkiyafanya mtawawahi wale waliokutangulieni na hakuna yeyote baada yenu atakayekudirikini na nyinyi ndio ambao mtakuwa wabora katika wale walio kati yao isipokuwa ambaye atafanya mfano wake. Leteni Tasbiyh, Tahmiyd na Takbiyr mara 33 baada ya kila swalah.” Tukatofautiana baina yetu. Baadhi yetu wakasema: “Tulete Tasbiyh mara 33, Tahmiyd mara 33 na Takbiyr mara 33.” Nikarejea kwake. Akasema: “Sema:

سُـبْحانَ الله

”Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu.”

الحَمْـدُ لله

”Himdi zote njema anastahiki Allaah.”

واللهُ أكْـبَر

”Allaah ni mkubwa.”

Kwa kila moja katika hizo mara 33.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

124 – Ka´b bin ´Ujrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maneno yanayofuatana ambayo hakhasiriki mwenye kuyasema au mwenye kuyasema baada ya kila swalah ya faradhi; Tasbiyh mara 33, Tahmiyd mara 33 na Takbiyr mara 34.”[2]

Ameipokea Muslim.

125 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kumsabihi Allaah baada ya kila swalah mara 33, akamuhimidi Allaah mara 33, akamkabiri Allaah mara 33 ambazo jumla inakuwa 99, na akakamilisha mia moja kwa kusema:

لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌم

“Hapana mwabudiwa isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana na mshirika. Ufalme Wake na himdi Zake na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.”,

basi atasamehewa makosa yake ingawa ni mfano wa povu la bahari.”[3]

MAELEZO

Katika Hadiyth hizi kuna sampuli tatu ya Dhikr baada ya kuswali. Tasbiyh baada ya swalah imekuja kwa aina zifuatazo:

1 – Atamsabihi Allaah mara 33, atamuhimidi Allaah mara 33 na kumkabiri Allaah mara 33. Jumla inakuwa mara 99. Hakuna ziada ya kuleta Tahliyl.

2 – Atamsabihi Allaah mara 33, atamuhimidi Allaah mara 33 na kumkabiri Allaah mara 33. Jumla inakuwa mara 99. Atakamilisha mia kwa kusema:

لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌم

“Hapana mwabudiwa isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana na mshirika. Ufalme Wake na himdi Zake na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.”

Kuhusu namna, mswaliji anaweza kuleta Tasbiyh mara 33, baada yake akaleta Tahmiyd mara 33 na baada yake akaleta Takbiyr mara 33 kwa kuzifuatanisha, au pia anaweza vilevile kukusanya baina yazo.

3 – Akaleta Tasbiyh mara 33, Tahmiyd mara 33 na Takbiyr mara 34. Jumla inakuwa mia.

4 – Akaleta Tasbiyh mara 10, Tahmiyd mara 10 na Takbiyr mara 10. Hivyo ndivo ilivyokuja katika upokezi wa al-Bukhaariy kupitia kwa Abu Hurayrah na ndani yake kukatajwa:

“Sabihini baada ya kila swalah [mara] kumi, himidini [mara] kumi na kabirini [mara] kumi.”

5 – Akamsabihi Allaah mara 25, akamuhimidi Allaah mara 25, akaleta Tahliyl mara 25, akamkabiri Allaah mara 25. Jumla inakuwa mia moja.

Ili mtu aweze kusamehewa madhambi kwa nyuradi hizi ni sharti ajiepushe na madhambi makubwa.

[1] al-Bukhaariy (843) na Muslim (595).

[2] Muslim (596).

[3] Muslim (597).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 117-119
  • Imechapishwa: 09/11/2025