Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

22 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ambaye yatamshinda matapishi hakuna juu yake kulipa na ambaye atajitapisha basi alipe.”[1]

MAELEZO

Hadiyth hii ni dalili kuwa mwenye kufunga akitapika kwa kukusudia, basi swawm yake itabatilika na atalazimika kulipa. Haya ndio maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni. Shaykh-hul-Islaam Ibn Taymiyyah (ambaye pia anaonelea kuwa kutapika kunabatilisha swawm) ameielezea sababu ya hili kuwa kutapika kunafanya udhaifu wa mwili na kunatoa chakula au maji mwilini ambavyo mtu hufaidi katika mwili wake. Vilevile kikosi kikubwa cha wanazuoni wamejengea hoja kwa Hadiyth ya Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitapika kisha akafuturu…[2] Hata hivyo kuna majibu yaliyotolewa dhidi ya ushahidi huu:

1 – Hadiyth hii kuna maoni tofauti juu ya cheni yake ya wapokezi, kama walivyosema al-Bayhaqiy na wengine miongoni mwa wenye kuhifadhi.  al-Majd ameitaja katika ”al-Muntaqaa” kwa tamko:

”Alitapika ambapo akatawadha… ”

Akaiegemeza kwa Ahmad na at-Tirmidhiy na hakuna ndani wapokezi hao wawili, kama alivosema Ahmad Shaakir[3].

2 – Hili lilitokea katika swawm ya kujitolea na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitapika kisha akafuturu kwa sababu ya kudhoofika. Namna hii ndivo ilivyopokelewa katika baadhi ya Hadiyth hali ya kufasiriwa. Hayo yametajwa na at-Tirmidhiy. Ibn Battwaal amesema:

”Hadiyth hii haina dalili kuwa kutapika kulimfunguza, bali inaonyesha kuwa alitapika kisha baadaye akafuturu.”[4]

3 – Hiki ni kitendo tu, jambo ambalo halifahamishi kuwa ni lazima kufanya hivo.

[1] Ahmad (2/498), Abu Daawuud (2380), at-Tirmidhiy (720), an-Nasaa’iy (3119) na Ibn Maajah (1676).

[2] Tazama ”as-Sunan al-Kubraa” (04/220) na “al-Majmuu” (06/54-55).

[3] Jaamiy’ at-Tirmidhiy (01/143).

[4] Sharh Ibn Battwaal (04/81).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/53-54)
  • Imechapishwa: 25/02/2025