40. Anayepinga kitu katika majina na sifa za Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

                                                        وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَنِ

“… ilihali wao wanamkanusha Mwingi wa rehema.” (ar-Ra´d 13:30)

2- al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Waelezeni watu kwa wanayoyajua. Je, mnataka akadhibishwe Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?”[1]

3- ´Abdur-Razzaaq amepokea kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Ibn Twaawuus, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Ibn ´Abbaas ambaye alimuona mtu akisisimka wakati aliposikia Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliotaja sifa za Allaah akiwa ni mwenye kulipinga hilo ambapo akasema:

“Ni kitu gani kinachowatia woga watu hawa? Wanafanya woga kwa Aayah zilizo wazi ilihali wanaegemea Aayah sizizokuwa waz.”[2]

Pindi Quraysh walipomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitaja Mwingi wa rehema wakapinga hilo. Ndipo Allaah akateremsha juu yao:

وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَنِ

“… ilihali wao wanamkanusha Mwingi wa rehema.”

MAELEZO

Mlango huu mwandishi ameutunga kwa ajili ya kubainisha uwajibu wa kuthibitisha majina na sifa za Allaah kwa njia inayolingana Naye (Subhaanahu wa Ta´ala) pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna, kuzifananisha wala kuzigeuza. Mtu hatakiwi kudhanganyika na maoni ya Mu´tazilah na watu wa batili wengine. Ni wajibu kwake kuchukua yale yaliyosemwa na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika Maswahabah na wale waliofuata mwenendo wao. Hii ndio ´Aqiydah iliofikishwa na Mitume. Wote walikuwa ni wenye kuthibitisha majina na sifa za Allaah kwa njia inayolingana Naye. Maswahabah na wale wote waliowafuata kwa wema walizipitisha Aayah na Hadiyth zinazozungumzia sifa kama zilivyokuja na wakathibitisha zile dalili za majina na sifa. Yote hayo kwa ajili ya kutendea kazi maneno Yake Allaah:

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ اللَّهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Sema: “Yeye ni Allaah – Mmoja pekee, Allaah aliyekamilika, mkusudiwa wa haja zote. Hakuzaa na wala hakuzaliwa, na wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.” (al-Ikhlaasw 112:01-04)

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

”Basi msimpigie Allaah mifano! Hakika Allaah anajua nanyi hamjui.” (al-Israa´ 16:74)

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (ash-Shuuraa 42:11)

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua yeyote mwenye jina kama Lake?” (Maryam 19:65)

 Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hana Mwenye jina kama Lake wala anayelingana Naye.

Kuhusu Jahmiyyah wao wamekanusha majina na sifa za Allaah na wakayapindisha majina. Maoni yao yanapelekea kukanusha kabisa kabisa uwepo wa Allaah. Kwa ajili hiyo ndio maana Ahl-us-Sunnah wamewakufurisha. Ni wajibu kuwaua ikiwa hawakutubia. Wanatakiwa kuambiwa kutubia kwa sababu ya kupinga kwao yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah na maafikiano. Mwandishi ametaja kichwa cha khabari kwa kutokufungamanisha pasi na kumhukumu yule mwenye kukanusha majina na sifa za Allaah. Hata hivyo hukumu yake ni kwamba ni kafiri.

 1- Allaah (Ta´ala) amesema:

                                                        وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَنِ

“… ilihali wao wanamkanusha Mwingi wa rehema.”

Allaah (Ta´ala) amebainisha kwamba Mwingi wa rehema ndio Mola na Mungu wetu na kwamba yule mwenye kumkufuru Mwingi wa rehema basi amemkufuru Allaah. Kwa hivyo ni wajibu kwa muumini kutahadhari na sifa za wapotevu hawa na afuate mwenendo wa wanachuoni na waumini. Allaah ameonelea kule kukanusha kwao sifa hii ni kumkufuru Mwingi wa huruma na ni dalili inayofahamisha kwamba mwenye kukanusha sifa amekufuru.

2- al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Waelezeni watu kwa wanayoyajua. Je, mnataka akadhibishwe Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?”

Mtu ambaye anawawaidhi na kuwakumbusha wengine basi anatakiwa kutumia matamshi na usulubu wanaoutambua ili waweze kustafidi na kufaidika. Kila watu wana usulubu wao. Ukiwazungumzisha watu kwa njia wasiyoitambua basi kuna khatari wakaja kukufahamu vibaya. Haijalishi kitu maudhui yanahusiana na majina, sifa au hukumu za Allaah. Haijalishi kitu lugha unayozungumza ni kiarabu, kingereza, urdu au lugha nyingine. Hata waarabu wenyewe wanaelewa tofauti. Zungumza na watu wote kwa njia waliyozowea ili waweze kukifahamu kile unachokisema na ili wasije kumkadhibisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Wale wanaomkadhibisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika sifa za Allaah wako katika khatari kubwa. Kwa sababu wamezipindisha sifa za Allaah kinyume na tafsiri zake na wamezizungumzia kwa njia isiyostahiki mpaka mwishowe wakazikanusha. Wengi wao kuna uwezekano wakawa wamezifahamu kimakosa kwa sababu sio waarabu. Baadhi ya Salaf wamesema kuwa ´Amr bin ´Ubayd amesema kuwa watenda madhambi watadumishwa Motoni milele kwa sababu Allaah kawaahidi hilo. Ndipo Salaf wakamwambia kwamba Allaah anaweza kuvunja ahadi ya adhabu na hawezi kuvunja ahadi ya thawabu. Kuvunja ahadi ya adhabu ni utukufu na kuvunja ahadi ya thawabu ni kusemwa vibaya. Ndipo wakamwambia:

“Umetumbukia katika hayo kwa sababu sio mwarabu.”

Bi maana unadhani kuwa ni jambo baya kuvunja ahadi ya adhabu. Si kweli. Mshairi amesema:

Mimi nikiahidi kumuadhibu au kumlipa

nitaivunja ahadi yangu ya kumuadhibu na kutimiza ahadi yangu ya kumlipa

Hii ni sifa.

3- ´Abdur-Razzaaq amepokea kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Ibn Twaawuus, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Ibn ´Abbaas ambaye alimuona mtu akisisimka wakati aliposikia Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliotaja sifa za Allaah akiwa ni mwenye kulipinga hilo ambapo akasema:

“Ni kitu gani kinachowatia woga watu hawa? Wanafanya woga kwa Aayah zilizo wazi ilihali wanaegemea Aayah sizizokuwa waz.”

Pindi Quraysh walipomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitaja Mwingi wa rehema wakapinga hilo. Ndipo Allaah akawateremshia juu yao:

وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَنِ

“… ilihali wao wanamkanusha Mwingi wa rehema.”

Wakati wanaposikia Aayah za wazi na Hadiyth wanasikia woga na wanakuwa na unyenyekevu. Wanaposikia Aayah kuhusu sifa za Allaah zinawatatiza na wanaangamia kwa sababu ya kutatizika na kukanusha. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa jambo hili ni la tokea hapo kale na kwamba kitu kama hicho kilikuwepo tokea hapo wakati wa Maswahabah. Wanaangamia kwa sababu ya Aayah za Qur-aan na Hadiyth ambazo wanaona kuwa haziko wazi na wanazitilia mashaka. Ni dalili inayofahamisha kwamba kupinga na kutilia mashaka yale Allaah aliyowabainishia waja Wake ni maangamivu.

Haki ni kuamini yale yote yaliyokhabarishwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ukifahamu kilichosemwa, ni jambo zuri na himdi zote ni za Allaah, na kama bado hujafahamu, basi unachotakiwa kusema ni kwamba Allaah ndiye mjuzi zaidi na uwaulize wanachuoni. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yale yote yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah. Wameridhishwa nayo na wanayatendea kazi. Pindi wanapokutana na kitu ambacho kimewatatiza basi wanakirudisha katika zile Aayah ambazo ziko wazi na bainifu na kwa njia hiyo wanakifahamu. Hawaifanyi Qur-aan wala Sunnah kuwa ni vyenye kugongana. Hawatilii mashaka. Wanatambua kuwa yale maandiko ambayo hayako wazi hayapingani na yale yaliyo wazi. Bali uhakika wa mambo yale maandiko yasiyokuwa wazi ni sehemu ya yale yaliyo wazi. Yale yote ambayo hawakuyafahamu wanamwacha Yeye ambaye anayajua yaliyofichikana ayashughulikie ambaye ni Allaah (Subhaanah). Kuhusu maana yake ni yenye kufahamika katika lugha ya kiarabu ambayo Allaah amewazungumzisha watu kwayo. Kwa ajili hiyo Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipoulizwa swali kuhusu kulingana kwa Allaah:

“Kulingana kunatambulika. Namna haijulikani. Kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah.”

Bi maana ni Bid´ah kuuliza kuhusu namna. Amebainisha (Rahimahu Allaah) kwamba kulingana kunatambulika na kwamba namna haitambuliki.

Faida:

Mwenye kusema kwamba Pepo na Moto vitatokomea/vitakwisha ni kafiri. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَأَمَّا الَّذِينَ سُعِدُوا فَفِي الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۖ عَطَاءً غَيْرَ مَجْذُوذٍ

“Ama wale walio furahani, basi watakuwa katika mabustani, ni wenye kudumu ndani yake zitakavyodumu mbingu na ardhi isipokuwa atakavyo Mola wako – ni hiba isiyokatizwa.” (Huud 11:108)

لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ

“Hautowapata ndani yake uchovu nao humo hawatotolewa.” (al-Hijr 15:48)

Kadhalika ni kosa kusema kwamba Moto utakwisha. Maoni sahihi walionayo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba Moto hautakwisha.

Faida:

Waislamu wamekubaliana juu ya kwamba ardhi imetulizana na jua ndio linalozunguka. Wale wanaosema kwamba ardhi ndio inayolizunguka jua wanachomaanisha ni kwamba ardhi ndio iliyotulizana, jambo ambalo ni kufuru:

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ

“Na jua linatembea hadi matulio yake, hayo ni matengenezo ya Mwenye nguvu kabisa, mjuzi.” (Yaa Siyn 36:38)

[1] al-Bukhaariy (129).

[2] al-Muswannaf (20895). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (485).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 127-129
  • Imechapishwa: 31/10/2018