39. Kitu kinachopewa nafasi ya mbele kabisa kwa wanafunzi wa kweli

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ni vipi muqtadha hii kubwa inaweza kupotea kwa zile karne zote ambazo ni bora? Kitu kama hicho hakipatikani hata kwa yule kiumbe ambaye ni mpumbavu kupindukia, mpuuzaji zaidi, amezama zaidi katika kuitafuta dunia na ambaye amepumbaa zaidi na kumdhukuru Allaah.

MAELEZO

Kinachopelekea ni kuitafuta haki. Kuwa na ujinga na kumpuuza Allaah (´Azza wa Jall) ni mambo yanayofanywa na watu waliopumbaa na watu wa matamanio, watu wenye tamaa juu ya dunia. Kuhusu watu wanaotafuta elimu sahihi na maarifa ya haki maudhui haya ni miongoni mwa vitu wanavyovipa kipaumbele kabla ya kingine chochote, wanaoshika nafasi ya mbele kabisa ni Maswahabah wa Mtume  wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na vile vizazi bora. Hawa hamu yao kubwa ilikuwa kumtambua Allaah na yale yote yanayowafanya kumkurubia na kuitafuta Aakhirah. Kuhusu watu wa dunia, watu wa matamanio na watu wapuuzi ni kama alivosema Allaah (´Azza wa Jall):

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ ۚ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ ۖ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا

“Je, unadhania kwamba wengi wao wanasikia au wanatia akilini? Si vyenginevyo isipokuwa ni kama wanyama, bali wao wamepotea zaidi njia!”[1]

Hakuna wanachojali isipokuwa matamanio yao tu. Wao ni kama wanyama ambao hakuna wanachotamani isipokuwa tu kula na kunywa. Bali wao ni wapotofu zaidi kuliko wanyama, kwa sababu wanyama hawakufaradhishiwa kufanya ´ibaadah. Wanyama hawasubiriwi na Pepo wala Moto. Watu hawa wamepuuza mustakabali na maisha yao ya huko Aakhirah. Wanyama wao hawana Aakhirah. Wanaishi tu hapa duniani. Wameumbwa kwa ajili ya manufaa ya watu. Wao hawatofanyiwa hesabu wala Pepo wala Moto. Siku ya Qiyaamah Allaah atawaamrisha wawe mchanga – na watakuwa hivyo. Ama mtu huyu atafufuliwa kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa, ima atakuwa miongoni mwa watu wa Peponi au miongoni mwa watu wa Motoni. Aakhirah hatokufa kamwe. Wakazi wa Peponi watadumishwa Peponi milele, na wakazi wa Motoni ambao ni makafiri na washirikina watadumishwa Motoni milele. Ni vipi mtu mwenye akili ndogo kabisa ataweza kughafilika juu ya uhalisia huu? Na ni vipi atayajua haya pasi na kuijua ´Aqiydah iliyosalimika ambayo imejengeka juu ya msingi wa imani, kukiwemo kuamini siku ya Qiyaamah?

[1] 25:44

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 05/08/2024