Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Hakuna kitu ambacho nafsi zilizosalimika zinakitamani mno kama kutambua suala hili. Hilo ni jambo linalotambulika kimaumbile.

MAELEZO

Hakuna kitu ambacho nafsi zilizosalimika inakitamani mno kama kutambua majina na sifa za Allaah na kumpwekesha, ´Aqiydah wanayoitakidi juu ya Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuwa na utambuzi juu ya Allaah (´Azza wa Jall), utukufu na ukubwa Wake. Hayo ndio mambo ambayo nafsi inayatamani zaidi. Kwa sababu ukimtambua Mola wako, basi unampenda na unamwabudu. Unataka kujikurubisha Kwake. Ukijua ukubwa, uwezo, utukufu, rehema, ukali wa kulipiza Kwake kisasi na ukali wa ghadhabu Zake, basi hapo unafanya kila ukiwezacho kujikurubisha Kwake kwa yale anayoyapenda na unajiepusha na yale yote yanayomghadhibisha na kumkasirisha. Hakuna kitu nafsi inakipenda zaidi kama jambo hili.

Ni vipi utamwabudu Mola usiyemtambua na wala hujui majina na sifa Zake? Huyu ni mola asiyetambulika. Lakini ukimjua kwa majina, sifa, alama na viumbe Wake yatakufahamisha juu ya ukubwa Wake na kwamba Yeye ndiye anastahiki kuabudiwa. Unapotafakari juu ya uumbaji wa mbingu, ardhi na yale mambo ya ajabu yanayopatikana ndani yake, basi utasema kama wanavosema waumini wengine wote:

رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

“Ee Mola wetu! Hukuumba haya bure – kutakasika ni Kwako tukinge na adhabu ya Moto!”[1]

Utamjua Allaah na ukubwa Wake wakati unapowatazama viumbe Wake. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ambaye ameweza kuumba viumbe hivi vikubwa na vingi vinafahamisha ukubwa, uwezo, ujuzi na hekima Yake. Kwa hivyo utamjua Mola wako (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa alama na sifa Zake.

[1] 3:191

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 69-70
  • Imechapishwa: 05/08/2024