38. Sura ya tatu: Radd kwa mwenye kupinga majina na sifa au akapinga kitu katika hayo

Kuna sampuli tatu ya wale wanaopinga majina na sifa za Allaah:

1- Jahmiyyah: Hawa ni wale wafuasi wa Jahm bin Swafwaan. Hawa wanapinga majina na sifa zote za Allaah.

2- Mu´tazilah: Hawa ni wale wafuasi wa Waaswil bin ´Atwaa’ ambaye alijitenga na kikao cha al-Hasan al-Baswriy. Hawa wanathibitisha majina peke yake yasiyokuwa na maana. Wanapinga sifa zote.

3- Ashaa´ira, Maaturiydiyyah na vifaranga vyao. Hawa wanathibitisha majina na baadhi ya sifa na wanapinga zengine. Utata ambao wote wameyajenga madhehebu yao juu yake ni eti kukimbia kumfananisha Allaah na viumbe Wake. Hoja yao ni kwamba viumbe wanaitwa kwa baadhi ya majina hayo na wanasifika kwa sifa hizo. Hivyo wanaona ushirikiano katika tamko la jina na sifa na maana zake unapelekea kushirikiana katika uhakika wa mawili hayo. Kwa hivyo wanaona kuwa jambo hilo litapelekea kuwafananisha viumbe na Muumba. Baada ya jambo hilo wakalazimiana na moja katika mambo mawili:

a) Ima kuyapindisha maana maandiko ya majina na sifa za Allaah kutoka katika udhahiri wake.

b) Ima kutegemeza maana ya maandiko haya kwa Allaah na wakasema kuwa Allaah pekee ndiye mjuzi wa alichokusudia na wakati huohuo kuamini kwamba hayako kwa udhahiri wake.

Watu wa kwanza waliotambulika kupinga majina na sifa za Allaah ni baadhi ya washirikina wa kiarabu ambao Allaah aliteremsha juu yao maneno Yake (Ta´ala):

كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَاكَ فِي أُمَّةٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهَا أُمَمٌ لِّتَتْلُوَ عَلَيْهِمُ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَـٰنِ

“Hivyo ndivyo Tumekutuma katika Ummah uliokwishapita kabla yake nyumati zengine ili uwasomee yale tuliyokufunulia Wahy, nao wanamkufuru ar-Rahmaan.”[1]

Sababu ya kuteremka Aayah hii ni kwamba Quraysh walipomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitaja Mwingi wa huruma (ar-Rahmaan) wakapinga hilo. Ndipo Allaah akateremsha juu yao:

وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَـٰنِ

“… nao wanamkufuru ar-Rahmaan.”

Ibn Jariyr ametaja kwamba hayo yalipitika katika suluhu ya Hudaybiyah wakati mwandishi alipoandika kuhusu qadhiya ya suluhu iliopitika kati yao na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

بسم الله الرحمن الرحيم

“Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”

 Ndipo Quraysh wakasema:

“Kuhusu Mwingi wa rehema sisi hatuitambui.”

Ibn Jariyr amepokea vilevile kupitia kwa Ibn ´Abbaas aliyesimulia kwamba: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba du´aa hali ya kusujudu akisema:

‏يا رحمن يا رحيم

“Ee Mwingi wa rehema, ee Mwenye kurehemu.”

Ndipo washirikina wakasema:

“Huyu anadai kuwa anamuomba Mmoja. Hivi sasa anawaomba wawili.” Ndipo Allaah akateremsha:

قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ

“Sema: “Muiteni Allaah au muiteni ar-Rahmaan”, vovyote mtakavyomwita basi [tambua kuwa] Yeye ana majina mazuri kabisa.”[2]

Amesema (Ta´ala) katika Suurah “al-Furqaan”:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اسْجُدُوا لِلرَّحْمَـٰنِ قَالُوا وَمَا الرَّحْمَـٰنُ

“Wanapoambiwa: “Msujudieni ar-Rahmaan”, basi husema: “Ni nani huyo ar-Rahmaan?”[3]

Washirikina hawa ndio watangu wa Jahmiyyah, Mu´tazilah, Ashaa´irah na kila mwenye kumkanushia Allaah yale aliyojithibitishia Mwenyewe au aliyothibitishiwa na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika majina na sifa za Allaah. Waovu walioje waliotangulia kwa waovu walioje waliokuja baadaye!

[1] 13:30

[2] 17:110

[3] 25:60

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 69-70
  • Imechapishwa: 05/03/2020