38. Mfungaji anapaswa kuithamani swawm yake

Hadiyth hizi zinafahamisha kuwa ni jambo lililosisitizwa kwa mwenye kufunga kuithamini swawm yake na kuilinda. Ikiwa mtu atamshambulia kwa kumpiga au kumtukana basi haifai kwake kumrudishia, japokuwa kulipiza kisasi kunajuzu. Lakini katika hali ya swawm anajizuia na anasema kuwa amefunga. Ikiwa kulipiza kisasi hakufai katika hali hii, basi kuanzisha uadui ndiyo haramu zaidi na dhambi yake ni kubwa zaidi, kwa kuwa kudhulumu ni haramu katika kila wakati. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَعْتَدُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

“… na wala msichupe mipaka. Hakika Allaah hawapendi wenye kuchupa mipaka.”[1]

Kufanya uadui katika hali ya swawm ni jambo chafu zaidi na dhambi yake ni kubwa zaidi. Kwa hiyo ni wajibu kwa mfungaji kuuzuia ulimi wake na maneno yasiyo na kheri ikiwa ni pamoja na uongo, kusengenya, umbea, kutukana na kila maneno mabaya. Vivyo hivyo ajizuie yeye mwenyewe na mwili wake dhidi ya matamanio na mambo yote yaliyo haramu. Haya yote yanaingia katika ueneaji wa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yule asiyeyaacha maneno ya uongo na kuufanyia kazi, basi Allaah hana haja ya yeye kuacha chakula chake na kinywaji chake.”[2]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”… asifanye maneno machafu wala ufuska.”

Siri ya funga ni kuizuia nafsi dhidi ya matamanio na kupata uwezo wa kujilinda nafsi dhidi ya shaytwaan na wasaidizi wake. Mkono wake uwe mtupu na asitembee kwa miguu kwenda katika batili. Wanazuoni wamesema kwamba kusengenya, kama kunavyokuwa kwa ulimi, hakuna tofauti kati yake na kufanyika kwa macho, mikono au midomo. Mwenye kufunga hapati ujira wa swawm yake kwa sababu ya dhambi zake, hata kama swawm hiyo haijabatilika Kishari´ah, kwa kuwa hapati thawabu ilihali anapata taabu ya njaa na kiu kwa sababu hakutekeleza swawm ya kweli, nayo ni ile inayomlazimu Kishari´ah kuacha mambo yaliyo haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemwamrisha mwenye kufunga anapotukanwa aseme:

”Mimi ni mwenye kufunga.”

Kwa dhahiri ni kwamba atamke hilo kwa maneno yake mwenyewe ili amjuze kile kinachomzuia kujibu tusi, nacho ni swawm. Kwa njia hiyo anakata shari, anajikumbusha yeye mwenyewe na anamkumbusha aliyetukana heshima ya swawm, jambo ambalo humzuia adui yake kwa njia iliyo bora zaidi.

[1] 02:190

[2] al-Bukhaariy (1903).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 09/03/2026