Kisha akasema[1]:

”Ama kutajwa kwa siku ya Qiyaamah katika Hadiyth, basi hiyo ni kwa sababu hiyo ndiyo siku ya malipo. Humo inaonekana wazi uzito wa harufu hiyo ya kinywa kwenye mizani kuliko harufu ya miski inayotumika duniani kwa ajili ya kuondoa harufu mbaya ili kutafuta radhi za Allaah (Ta´ala) kwa kuamrishwa kuepukwa na harufu mbaya na kutumika harufu nzuri kama kwenye misikiti, swalah na ´ibaadah nyingine. Basi siku ya Qiyaamah ikatajwa kwa kutolewa mfano, kama ambavyo imetajwa katika maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّهُم بِهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّخَبِيرٌ

”Hakika Mola wao siku hiyo kwao ni Mjuzi wa khabari za dhahiri na siri.”[2]

Baadhi ya mapokezi yametaja kwa njia isiyofungamana kutokana na kwamba msingi wa ubora wa harufu hiyo ni thabiti katika dunia na Aakhirah.”

Inashangaza kumraddi kwake Abu Muhammad kwa jambo ambalo si yeye Abu Muhammad wala mwengine yeyote halikatai, kwani alichokitafsiri kuwa kupendezwa kwa harufu hiyo duniani kuwa ni sifa nzuri ya Allaah kwa wanaofunga na radhi Yake kwa kitendo chao ni jambo lisilopingwa na muislamu yeyote. Hakika Allaah (´Azza wa Jall) amewasifia katika Kitabu Chake na katika yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaridhia kwa kitendo chao. Basi ikiwa hiyo ndiyo tafsiri ya kupendezwa huko, basi Shaykh Abu Muhammad (Rahimahu Allaah) hawezi kulipinga. Alichokitaja Shaykh Abu Muhammad (Rahimahu Allaah) ni kwamba harufu hiyo itaonekana uzuri wake kulinganisha na harufu ya miski siku ya Qiyaamah kama inavyoonekana uzuri wa damu ya mashahidi na kuwa kama harufu ya miski. Bila shaka hilo ni siku ya Qiyaamah, kwani aliyefunga siku hiyo atakuja huku harufu ya kinywa chake ikiwa nzuri zaidi kuliko harufu ya miski, kama vile majeruhi wa jihaad atakavyokuja na huku harufu ya damu yake ikiwa kama miski. Hili ni bayana zaidi kwani jihaad ni bora kuliko swawm. Ikiwa uzuri wa harufu hiyo ya majeruhi utaonekana tu siku ya Qiyaamah, basi ndivyo ilivyo kwa aliyefunga.

Ama Hadiyth ya Jaabir inayosema:

“Wanapofikia jioni harufu ya vinywa vyao ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”

Hii ni jumla ya hali siyo ya khabari. Ikiwa jumla hiyo ni ya hali, basi Abu Muhammad ana haki kusema kwamba ni hali ya kutarajiwa. Hali kama hiyo inaweza kucheleweshwa baada ya wakati wa tendo linaloihusisha. Kwa ajili hiyo lau ingelitamkwa wazi:

“… wanapofikia jioni na harufu ya vinywa vyao ni nzuri kuliko miski siku ya Qiyaamah.”,

basi usomaji huo usingekuwa batili. Ni kama vile kusema ”… wanapofikia jioni na hilo ni kwao siku ya Qiyaamah.”

Kuhusu maneno yake:

“Harufu ya kinywa cha aliyefunga wakati inapobadilika… ”

Huu ni wakati unaothibitisha au kufafanua mwanzo wa maneno au kuonyesha kuwa maana halisi ndiyo inayokusudiwa, siyo ya kinaya wala ya sitiari. Hii ni sawa na kusema “Jihaad ya muumini wakati anapopigana na swalah yake wakati anaposwali” Allaah humlipa kwa hiyo siku ya Qiyaamah na humpandisha daraja kwa hiyo.” Hili linakaribiana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mzinifu anapozini hali ya kuwa ni muumini wala hanywi pombe mlevi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini.”

Makusudio si kwamba imani hupotea tu wakati anapofanya tendo hilo la madhambi kwa namna ya kwamba ikikamilika tendo hilo na likaisha, basi imani yake hurudi. Bali hilo linamwandama hadi atakapofanya tawbah ya kweli. Vinginevyo muda wa kuwa ni mwenye kuendelea kufanya hivo hata kama hakulifanya tena kwa wakati huo, bado huchukuliwa kuwa ni mwenye dhambi na hukumu za madhambi hayo hubakia kwake hadi atakapofanya tawbah – na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye ajuaye zaidi.

[1] Ibn-us-Swalaah.

[2] 100:01

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 10/08/2025