35. Daima huja na hoja tata ili kuwatia watu mchanga wa machoni

Tunasema “Majibu kwa watu wa batili ni kwa njia mbili: Kwa jumla na kwa kina.”

Ama jibu la jumla, hakika ni jambo kubwa na faida kubwa kwa yule mwenye kulifahamu. Nalo ni maneno Yake (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

“Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayah zilizo wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo ni zenye kutatiza. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zenye kutatiza ili kutafuta fitina na kutaka kuzipotosha. Na hakuna ajuaye uhakika wake isipokuwa Allaah.” (03:07)

MAELEZO

Hapa anabainisha (Rahimahu Allaah) ya kwamba ataziraddi hoja tata hizi mbili kwa njia mbili:

1 – Njia ya jumla na ilioenea nzuri yenye kutosheleza kuraddi kila utata.

2 – Ya kina.

Namna hii ndivyo wanavyotakiwa wanachuoni kwenda pindi wanapojadili. Wanatakiwa kuja na jibu la kijumla ili liweze kufunika kile anacholenga mpinzani. Kadhalika wanatakiwa kuja na jibu la kina juu ya kila suala kivyake. Allaah (Ta´ala) amesema:

الر ۚ كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ

“Alif Laam Raa. Kitabu ambacho Aayah Zake zimetimizwa barabara, kisha zikafasiliwa kutoka kwa Mwingi wa hekima, Mjuzi wa yaliyodhahiri na yaliyofichikana.” (11:01)

Katika jibu la kijumla ametaja (Rahimahu Allaah) ya kwamba wale ambao wanafuata Aayah zisizokuwa wazi maana yake ndio wale ambao nyoyoni mwao mna upotevu. Hilo limethibiti pia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ

“Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayah zilizo wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo ni zenye kutatiza. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zenye kutatiza ili kutafuta fitina na kutaka kuzipotosha.”

Kwa ajili hii ndio maana utaona watu waliopinda siku zote huja na Aayah zisizokuwa wazi maana yake ili kuwatia watu mchanga wa machoni. Mfano wa hilo wanasema:

“Allaah (Ta´ala) sehemu hii amesema kadhaa na ile sehemu nyingine amesema kadhaa. Inakuweje?”

Haya ni mfano wa yale yaliyomfikia Naafiy´ bin al-Azraq pamoja na Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). as-Suyuutwiy ametaja mjadala wao katika “al-Itqaan” na kuna uwezekano akawepo mwengine aliyefanya hivo, kwa sababu ni wenye faida.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 11/11/2023