Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wataotoka Motoni baada ya kuungua na kuwa majivu. Watapelekwa kwenye mto karibu na mlango wa Pepo, kama ilivyopokelewa katika upokezi. Yatapitika namna anavyotaka Allaah na kama anavyotaka Allaah. Si vyengine isipokuwa inahusiana na kuamini na kusadikisha hilo.”

MAELEZO

Uombezi umethibiti kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Utapitika katika uwanja wa mkusanyiko siku ya Qiyaamah pindi watu watapokuwa wamezidiwa na woga kwelikweli. Wataenda kwa Aadam, kisha Nuuh, kisha Ibraahiym, halafu Muusa na mwishowe ´Iysaa. Kila mmoja katika wao ataomba udhuru kama inavyotambulika katika Hadiyth. Hatimaye jambo litaangukia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo atasema:

“Mimi ndiye mwenye haki nayo.”

Ataenda na kuanguka hali ya kusujudu chini ya ´Arshi. Atabaki hivo kwa muda mrefu. Atamsifu Allaah kwa sifa ambazo alikuwa hazijui katika maisha haya. Ni sifa ambazo Allaah atamfunza katika wakati huo. Halafu ataambiwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Inua kichwa chako. Uliza utapewa, omba utakubaliwa.”[1]

Atawaombea vilevile watu waliopata ngazi za chini ili waweze kupewa ngazi za juu ambapo Allaah atazinyanyua ngazi zao.

Atawaombea pia watu waliokuwa wanastahiki kuingia Motoni kwa sababu ya madhambi yao makubwa ili wasiingie. Katika hili Mitume, Malaika na waja wema nao pia wataombea. Uombezi huu, na maombezi mengine, kama tulivyosema anashirikiana na Mitume, watu wakweli, waja wema na Malaika.

Hadiyth kuhusu uombezi ni nyngi sana na zimepokelewa kwa mapokezi mengi. Baadhi yake zimepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim na khaswa khaswa Muslim. Moja katika hizo ni Hadiyth ijulikanayo ya Abu Sa´iyd ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtoe Motoni yule ambaye moyoni mwake kulikuwa imani sawa na uzito wa kipande cha dhahabu, kisha yule ambaye moyoni mwake kulikuwa imani sawa na uzito nusu ya kipande cha dhahabu, halafu yule ambaye moyoni mwake kulikuwa imani sawa na uzito wa mizizi ya tende moja, halafu yule ambaye moyoni mwake kulikuwa imani sawa na uzito wa mdudu chungu kisha yule ambaye moyoni mwake kulikuwa imani chini, chini na chini zaidi kuliko mdudu chungu.”[2]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atawatoa  wapwekeshaji kutoka Motoni kutokana na ile imani yao hata kama itakuwa ndogo kuliko uzito wa mdudu chungu, kama hayo yalivyothibiti katika Hadiyth Swahiyh.

[1] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

[2] al-Bukhaariy (7439) na Muslim (183).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 400-401
  • Imechapishwa: 10/09/2017