33. Harufu nzuri zaidi duniani na Aakhirah

Kuna ikhtilafu juu ya iwapo harufu hii hutokea kwa mfungaji katika dunia hii na katika Aakhirah. Kuna mitazamo miwili juu ya suala hili. Kulitokea mabishano kati ya wanazuoni wawili watukufu Abu Muhammad bin ´Abdis-Salaam na Abu ´Amr bin as-Swalaah kuhusu jambo hilo. Abu Muhammad alielemea kuwa hiyo ni harufu maalum kwa Aakhirah tu na akaandika kitabu kuunga mkono maoni hayo.

Abu ´Amr bin as-Swalaah akafuata njia ya Abu Haatim bin Hibbaan, kwani katika kitabu chake “as-Swahiyh” yake aliiwekea Hadiyth hii kichwa cha khabari kinachosema: “Tajulisho kwamba harufu ya kinywa cha mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah (Ta´ala) kuliko harufu ya miski.” Kisha akataja Hadiyth ya al-A´mash, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila tendo la mwanaadamu ni lake isipokuwa swawm. Swawm ni Yangu na Mimi ndiye nitakayeilipa. Hakika harufu ya kinywa cha mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski.”[1]

Kisha akaweka kichwa cha khabari kinachosema kwamba harufu ya kinywa cha mfungaji itakuwa nzuri zaidi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) siku ya Qiyaamah.” Kisha akataja Hadiyth nyingine kutoka kwa Ibn Jurayj, kutoka kwa ´Atwaa´, kutoka kwa Abu Swaalih az-Zayyaat, ambaye ameeleza kuwa amemsikia Abu Hurayrah akisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema: “Kila tendo la mwanaadamu ni lake isipokuwa swawm. Swawm ni Yangu na Mimi ndiye nitakayeilipa. Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake, hakika harufu ya kinywa cha mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah kuliko harufu ya miski. Mfungaji ana furaha mbili: anapofuturu hufurahi kwa futari yake na anapokutana na Allaah hufurahi kwa swawm yake.”

Abu Haatim amesmea:

”Alama ya waumini siku ya Qiyaamah ni mwangaza wa viungo vyao waliovitawadha navyo duniani, iwe ni tofauti kati yao na nyumati zingine, na alama yao siku ya Qiyaamah kwa ajili ya swawm yao ni harufu nzuri ya vinywa vyao. Harufu hiyo ikiwa bora zaidi kuliko harufu ya miski ili watambulike kati ya kundi hilo kwa sababu ya kitendo hicho. Allaah atujaalie tuwe miongoni mwao.”[2]

Kisha akaweka kichwa cha khabari mlango kuusu kwamba harufu ya kinywa cha mwenye swawm huenda ikawa pia ni kama harufu ya miski duniani. Kisha akasimulia kutoka kwa Shu’bah, kutoka kwa Sulaymaan, Dhakwaan, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Kila jema analolifanya mwanadamu hupewa thawabu mara kumi mpaka mara mia saba. Allaah (´Azza wa Jall) anasema: ”Isipokuwa swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi ndiye nitakayeilipa. Anaacha chakula kwa ajili Yangu. Anaacha kunywa kwa ajili Yangu na Mimi ndiye nitakayeilipa. Kwa mwenye swawm kuna furaha mbili: furaha wakati wa kufuturu na furaha wakati anapokutana na Mola wake (´Azza wa Jall). Harufu ya kinywa cha mwenye swawm anapojizuilia na chakula ni bora zaidi kwa Allaah kuliko harufu ya miski.”[3]

[1] Ibn Hibbaan (3422).

[2] Ibn Hibbaan (3423).

[3] Ibn Hibbaan (3424).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 58-60
  • Imechapishwa: 09/08/2025