218 – Abu Bakr bin Abiy ´Attwaab al-A´yan na Ya´quub bin ´Ubayd wametuhadithia: Yahyaa bin Hammaad ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa Abaan bin Taghlib, kutoka kwa Fudhwayl al-Fuqaymiy, kutoka kwa Ibraahiym an-Nakha´iy, kutoka kwa ´Alqamah bin Qays, kutoka kwa ´Abdullaah, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hataingia Motoni yeyote mwenye uzito wa chembe ya imani. Hataingia Peponi yeyote mwenye uzito wa chembe ya kiburi.” Mtu mmoja akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Hakika mtu anapenda nguo yake iwe nzuri na kiatu chake kiwe kizuri.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Hakika Allaah (´Azza wa Jall) ni Mzuri na anapenda uzuri. Kiburi ni kukataa haki na kuwadharau watu.”[1]

Hili ni tamko la Hadiyth ya Ya´quub bin ´Ubayd.

219 – ´Abdur-Rahmaan bin Swaalih ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Muhammad al-Muhaaribiy ametuhadithia, kutoka kwa Muusa bin ´Ubaydah, kutoka kwa Zayd bin Aslam, kutoka kwa Jaabir, ambaye ameeleza kwamba Mu´aadh amesema:

”Ee Mtume wa Allaah! Je, ni katika kiburi kuwa mmoja wetu awe na nguo anayovaa, mnyama anayepanda na chakula anachowakusanya juu yake wenzake?” Akasema: ”Hapana. Lakini kiburi ni kubeza haki na kumdharau muumini. Nitawaambia tabia ambazo yeyote zitakazokuwa ndani yake basi si mwenye kiburi: Kufunga mguu wa mbuzi, kuvaa sufi, kupanda punda, kukaa pamoja na waumini mafukara na mmoja wenu ale pamoja na familia yake.”

220 – Ibn Jamiyl ametuhadithia: ´Abdullaah ametukahabrisha: Muusa bin ´Ulayy bin Rabaah ametukhabarisha: Nimemsikia baba yangu akisimulia kwamba ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Watu wa Motoni ni wale wenye kufanya kiburi bila ya sababu, wajeuri na wakusanyaji wafanyao kiburi ambao ni mabakhili. Watu wa Peponi ni wale wanyonge na wenye kukandamizwa.”[2]

221 – Ibn Jamiyl ametuhadithia: ´Abdullaah ametukhabarisha: Hishaam bin ´Urwah ametukahabrisha, kutoka kwa Muhammad bin al-Munkadir, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika wapendwa wenu zaidi kwetu na waliokaribu zaidi nasi katika Aakhirah ni wenye tabia njema miongoni mwenu. Hakika wenye kuchukiwa zaidi kwetu na walio mbali zaidi nasi ni wapiga porojo, wenye maneno ya kujikweza, wenye maneno ya kujiona na wenye kiburi.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Tumekwishajua wapiga porojo na wenye maneno ya kujikweza, basi hao wenye maneno ya kujiona ni nani?” Akasema: ”Wenye kiburi.”

222 – Ibn Jamiyl ametuhadithia: ´Abdullaah ametukhabarisha: Ma´mar ametukhabarisha, kutoka kwa Qataadah, ambaye amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ

”Wala usiwabeuwe watu.”[3]

”Kwa maana kugeuza mgongo mbali wakati mtu anapokuzungumzisha.”

223 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Sulaymaan bin Hayyaan al-Ahmar ametuhadithia, kutoka kwa Ibn ´Ajlaan, kutoka kwa ´Amr bin Shu´ayb, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa baba yake, aliyeeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Siku ya Qiyaamah wenye kiburi watakusanywa wakiwa kama vumbi dogo kwa mfano wa sura za wanaume. Utawapanda kila kitu cha udhalili. Kisha watasukumwa hadi gereza ndani ya Jahannam linaloitwa Buulas. Litawafunika moto wa nyuzi, watanyweshwa kutoka katika tope la wendawazimu; ambalo ni usaha wa watu wa Motoni.”[4]

[1] Muslim (147-149).

[2] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (1741).

[3] 31:18

[4] at-Tirmidhiy (2492), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh. Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2492).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 263-269
  • Imechapishwa: 26/03/2026