Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

54 – Endapo viumbe wote watakusanyika kuzuia kitu ambacho Allaah (Ta´ala) amekwishahukumu kutokea kwake, basi hawatoweza. Na endapo wote watakusanyika kukileta kitu ambacho Allaah (Ta´ala) hajahukumu kutokea kwake, basi hawatoweza. Wino wa kalamu umekauka kwa yatayotokea mpaka siku ya Qiyaamah. Yale yaliyomkosa mja, hayakuwa yenye kumpata, na yale yaliyompata hayakuwa yenye kumkosa.

55 – Mja anapaswa kutambua kwamba Allaah umetangulia ujuzi Wake juu ya kila kiumbe Chake. Akayakadiria yote hayo makadirio ya kukata na hakuna awezaye kuyachengua, kupingana nayo, kuyaondoa, kuyageuza, kuyapunguza wala kuyaongeza katika viumbe Wake katika mbingu na ardhi Zake. Hayo ni katika mafundo ya imani, misingi ya utambuzi na kutambua upwekekaji wa kuabudiwa kwa Allaah (Ta´ala) na uola Wake. Kama alivosema (Ta´ala) ndani ya Kitabu Chake:

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

”Ameumba kila kitu kisha akakikadiria kipimo sawasawa.”[1]

وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا

“Na amri ya Allaah daima ni makadirio yaliyokadiriwa.”[2]

Ole wake ambaye anamfanya Allaah (Ta´ala) kuwa mgomvi wake juu ya makadirio na kila mgonjwa wa moyo mwenye kujishughulisha na jambo hilo. Amejaribu kwa fikira yake kutafuta mambo ya siri yaliyofichikana na kuishilia kwa atakayoyasema kuwa mwongo na mtenda dhambi.

MAELEZO

Ni sehemu katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ee Kijana! Nitakufundisha maneno: Muhifadhi Allaah Naye atakuhifadhi. Muhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Ukiomba, basi muombe Allaah, ukitafuta msaada, basi tafuta kutoka kwa Allaah. Jua ya kwamba ikiwa taifa zima litaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika isipokuwa kwa kitu alichokwishakuandikia Allaah. Kadhalika wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, basi howatokudhuru isipokuwa tu kwa kitu alichokwishakuandikia. Kwani kalamu zimeshanyanyuliwa na sahifa zimeshakauka.”[3]

[1] 25:2

[2] 33:38

[3] Ahmad (1/307) na at-Tirmidhiy (2516) aliyesema: ”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 47-50
  • Imechapishwa: 29/09/2024