30. Upazaji sauti wa ´Umar mbele ya Mtume

´Abdullaah bin Abiy Mulaykah amesema:

”Walikaribia watu wawili wema, Abu Bakr na ´Umar, kuangamia wakati walipopaza sauti zao mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipowasili msafara wa Banuu Tamiym. Mmoja wao akamwashiria al-Aqra’ bin Haabis, ndugu wa Banuu Mujaashiy, mwingine akamwashiria mtu mwingine (ambaye Naafiy´ hakumbuki jina lake). Ndipo Abu Bakr akamwambia ´Umar: “Hukutaka isipokuwa kunipinga.” ´Umar akajibu: “Sikutaka kukupinga.” Sauti zao zikaja juu kuhusu jambo hilo ambapo Allaah  (Subhaanah) akateremsha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ

“Enyi walioamini! Msizinyanyue sauti zenu juu ya sauti ya Mtume na wala msiseme naye kwa sauti ya juu kama mnavyosemezana wenyewe kwa wenyewe kwa sauti za juu, yasije yakaporomoka matendo yenu nanyi hamhisi.”[1]

Ibn-uz-Zubayr akasema: ”Baada ya Aayah hii ´Umar hakuweza kuzungumza na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa atalazimika kumuuliza ni nini alichosema.” Hakusema kuhusu hilo kuhusu baba yake, kwa maana Abu Bakr.”[2]

[1] 49:02

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (7302), ndani yake kuna upokezi kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah, kutoka kwa ´Abdullaah bin az-Zubayr, at-Tirmidhiy (17/39), ambaye ametamka wazi kwamba ´Abdullaah bin Abiy Mulaykah ameyasikia hayo kutoka kwa ´Abdullaah bin az-Zubayr, Ahmad (4/6) na at-Twabariy (26/119), ambapo Naafiy´ amesimulia kuwa Ibn Abiy Mulaykah amemuhadithia, kutoka kwa Ibn-uz-Zubayr. Kwa msemo mwingine cheni ya wapokezi ni yenye kuungana, kama alivyoashiria hilo Haafidhw Ibn Hajar katika “Fath-ul-Baariy” (10/212).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Swalaah fiyn-Ni´aal, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 23/06/2025