Inapokuja katika jambo la swalah watu wamegawantika katika daraja tano:

1 – Swalah ya yule anayejidhulumu nafsi yake na mwenye kupuuzia. Huyu hupunguza katika wudhuu´ wake, nyakati za swalah, mipaka yake na nguzo zake.

2 – Swalah ya yule anayelinda nyakati zake, mipaka yake, nguzo zake za dhahiri na wudhuu´ wake. Hata hivyo amepuuza kupambana na nafsi yake dhidi ya wasiwasi. Basi hupelekwa na wasiwasi na mawazo.

3 – Swalah ya yule anayelinda mipaka, nguzo zake na akajitahidi katika kuondoa wasiwasi na mawazo. Huyu yuko katika mapambano na adui wake ili asiibe swalah yake. Basi yeye yuko katika swalah na jihaad.

4 – Swalah ya yule ambaye anapoinuka kwa ajili ya swalah, hukamilisha haki zake, nguzo zake, mipaka yake na moyo wake wote unazingatia mipaka yake na haki zake ili asipoteze kitu chake chochote. Bali hima yake yote imeelekezwa kuiimarisha ipasavyo, kuikamilisha na kuitimiza. Moyo wake umeshughulishwa na hali ya swalah na utumwa kwa Mola wake (Tabaarak wa Ta´ala) ndani yake.

5 – Swalah ya yule ambaye anapoinuka kwa ajili ya swalah, hufanya kama katika daraja ya nne, lakini pamoja na hayo, moyo wake umewekwa mbele ya Mola wake (´Azza wa Jall), akimwangalia kwa moyo wake, akimchunga, akiwa amejaa mapenzi na utukufu Wake. Ni kama kwamba anamuona na anamtazama. Na ule wasiwasi na hatua havipo tena, mapazia yameondolewa baina yake na Mola wake. Basi tofauti baina yake na wengine katika swalah ni kubwa sana kuliko tofauti baina ya mbingu na ardhi. Huyu ndani ya swalah yake amejishughulisha na Mola wake (´Azza wa Jall) na jicho lake limetulia kwake.

Daraja ya kwanza ni ya mwenye kuadhibiwa. Ya pili ni ya mwenye kuhesabiwa. Ya tatu amefutiwa madhambi. Ya nne anapata thawabu. Ya tano amekaribishwa kwa Mola wake kwa kuwa ana fungu katika wale waliowekwa furaha ya macho yao katika swalah. Kwa hiyo yule ambaye macho yake yalipata furaha kwa swalah hapa duniani, basi macho yake yatapata furaha kwa ukaribu wa Mola wake (´Azza wa Jall) huko Aakhirah na macho yake pia yatapata furaha kwa Allaah duniani. Ambaye macho yake yalipata furaha kwa Allaah, basi atalifurahisha kila jicho. Na ambaye jicho lake halikufurahishwa kwa Allaah (Ta´ala), basi nafsi yake hukatika vipande juu ya dunia kwa majuto. Imepokewa kwamba mja anapoinuka kuswali, basi Allaah (´Azza wa Jall) husema:

“Inueni mapazia baina Yangu na mja Wangu. Anapogeuka basi Husema: ”Yateremsheni hayo mapazia.”

Kutazama huku kumetafsiriwa kuwa ni kutazama kwa moyo mbali na Allaah (´Azza wa Jall) kwenda kwa mwingine. Basi anapotazama kwa mwingine, huteremshwa pazia baina yake na baina ya Mola wake na hapo huingia shaytwaan na kumletea mambo ya dunia na kumwonyesha katika mfano wa kioo. Lakini anapouelekeza moyo wake kwa Allaah na asigeuke, shaytwaan hawezi kuingilia kati baina ya Allaah (Ta´ala) na moyo huo. Shatwaan haingii isipokuwa pale pazia linapotokea. Hivyo akimkimbilia Allaah (Ta´ala) na kuleta moyo wake, basi shaytwaan hukimbia. Akigeuka, basi shaytwaan huhudhuria. Hivi ndivyo ilivyo hali yake na hali ya adui yake katika swalah.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 49-51
  • Imechapishwa: 06/08/2025