Kwa sababu hiyo wanazuoni wa watu wa Kitabu hutofautiana sana juu ya masuala kama haya, jambo ambalo hufanya baadaye wafasiri wakatofautiana. Mfano wa hayo ni makinzano yao kuhusu majina ya watu wa pango, rangi ya mbwa wao, idadi yao, aina ya mti wa fimbo ya Muusa, majina ya ndege ambao Allaah (Ta´ala) alimuhuishia Ibraahiym, kiungo gani cha ng´ombe ambacho alipigwa yule muuliwa wa wana wa israaiyl, aina ya mti ambao Allaah alimzungumzisha Muusa kwao na mengineyo ambayo Allaah ameyaficha ndani ya Qur-aan, kwa sababu faida yoyote ya kuyajua ambayo inarejea katika dini wala dunia yao. Hata hivyo inafaa kutaja makinzano yao. Kama alivosema (Ta´ala):

سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ ۖ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ ۚ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ ۗ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاءً ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا

”Watasema: ”Watatu na wanne wao ni mbwa wao na wengine wanasema: ”Watano, na wa sita wao ni mbwa wao” – kwa kuvurumisha hivyo bila ya kujua – na wengine wanasema: ”Saba na wa nane wao ni mbwa wao”. Sema: ”Hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu, hivyo basi usibishane nao kwa mengine isipokuwa yale tuliyokufunuliwa wahy, na wala usimuulize yeyote kuhusu khabari zao.”[1]

Aayah tukufu imebeba mafunzo ya adabu na mafunzo katika kushughulikia masuala kama haya. Allaah (Ta´ala) ameelezea aina tatu ya maono yao, ameyadhoofisha maono mawili ya kwanza na akanyamazia maoni ya tatu, jambo linalofahamisha kuwa ndio sahihi zaidi. Kwa sababu ingekuwa batili, basi Allaah angeliyakataa kama alivyoyakataa yale mawili ya mwanzo. Kisha Akatilia mkazo kwamba kujua idadi yao hakuna faida yoyote ile, kwa ajili hiyo inatakiwa kusema kwa mambo mfano wa hayo:

قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم

”Sema: ”Hakuna anayewajua isipokuwa wachache tu.”

Hakuna anayejua kuhusu idadi yao isipokuwa wachache waliopewa elimu hiyo na Allaah. Kwa ajili hiyo Akasema:

فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاءً ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا

”Usibishane nao kwa mengine isipokuwa yale tuliyokufunuliwa wahy, na wala usimuulize yeyote kuhusu khabari zao.”

Usijichoshe katika mambo yasiyo na faida na wala usimuulize yeyote katika wao kwa sababu wao wenyewe hawajui lolote isipokuwa tu kubahatisha.

[1] 18:22

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 13/04/2025