Hakika swalah hufuta madhambi ya yule anayetekeleza haki yake, kuitimiza kwa unyenyekevu wake na kusimama mbele ya Allaah (Ta´ala) kwa moyo wake na kwa kuelekea Kwake. Hivyo basi anapotoka katika swalah hiyo huhisi wepesi ndani ya nafsi yake na huhisi mizigo mizito kuwa imeondolewa juu yake. Hupata nguvu mpya, faraja na pumziko la roho, kiasi kwamba hutamani lau asingetoka humo, kwa kuwa hiyo ndiyo furaha ya jicho lake, raha ya roho yake, bustani ya moyo wake na mahala pake pa kupumzika katika dunia. Basi haachi kuhisi kana kwamba yuko katika kifungo na dhiki hadi aingie tena ndani ya swalah. Ndipo hupata faraja kwayo, si kutoka kwayo. Basi wapendao swalah husema tuswali na tupate faraja kwa swalah yetu, kama alivyosema kiongozi wao, mfano wao bora na Nabii wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Bilaal, tupumzishe kwa swalah.”

Hajasema:

“Tupumzishe kutoka katika swalah.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Furaha ya jicho langu imefanywa ndani ya swalah.”

Basi yule ambaye furaha ya jicho lake iko katika swalah, vipi jicho lake litapata furaha bila swalah? Vipi ataweza kuvumilia kuikosa? Swalah ya mtu huyu ambaye moyo wake uko ndani yake, na ambaye furaha ya jicho lake imo katika swalah, hiyo ndiyo hupaa juu na huwa na nuru na hoja mpaka humlaki nayo Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall), ambapo ikasema:

“Akulinde Allaah (Ta´ala) kama ulivyonilinda mimi.”

Kuhusu swalah ya mpotevu, aliyezembea katika haki zake, mipaka yake na unyenyekevu wake, basi hiyo hufungwa kama inavyofungwa nguo chakavu na kupigwa nayo uso wa mwenyewe. Husema:

“Akupoteze Allaah kama ulivyonipoteza mimi.”

Bakr bin Bishr amesimulia kutoka kwa Sa´iyd bin Sinaan, kutoka kwa Abuz-Zaahiriyyah, kutoka kwa Abu Shajarah, kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa), kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Hakuna muumini yeyote anayekamilisha wudhuu´ wake katika maeneo yake kisha akasimama kwa ajili ya swalah katika wakati wake ambapo akaitekeleza kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) bila kupunguza chochote katika wakati wake, kurukuu kwake, kusujudu kwake na alama zake, isipokuwa huelekezwa kwa Allaah (´Azza wa Jall) ikiwa nyeupe, yenye mwangaza, ambayo nuru yake huangaza baina ya mashariki na magharibi hadi ifike kwa Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall). Yule anayesimama kwa swalah bila kukamilisha wudhuu´ wake, akaichelewesha kutoka wakati wake na akaiba kurukuu na kusujudu na alama zake, basi huelekezwa juu yake ikiwa nyeusi, yenye giza, ambayo haitapita hata nywele ya kichwa chake, nayo husema:

‘Akupoteze Allaah kama ulivyonipoteza mimi. Akupoteze kama ulivyonipoteza mimi!”[1]

Basi swalah inayokubaliwa na matendo yanayokubaliwa ni ile ambayo mja huiswali kwa namna inavyomstahiki Mola wake (´Azza wa Jall). Ikiwa ni swalah inayomfaa Mola wake (Tabaaraka wa Ta´ala) na inayomstahiki, basi hiyo inakuwa yenye kukubaliwa.

[1] at-Twayaalisiy (586), al-Bazzaar (7/140 na 150) na ash-Shaashiy (1290-1291). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (301).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 46-48
  • Imechapishwa: 06/08/2025