Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Swawm bora baada ya Ramadhaan ni mwezi wa Allaah Muharram na swalah bora baada ya faradhi ni swalah ya usiku.”
Imekuja katika upokezi mwingine:
“… swalah ya katikati ya usiku.”[1]
Ameipokea Muslim.
MAELEZO
Hadiyth hii ni dalili ya fadhilah ya kufunga mwezi wa Allaah Muharram na kwamba kufunga mwezi huu kunakuja mara moja baada ya mwezi wa Ramadhaan katika daraja ya ubora. Fadhilah ya kufunga mwezi huu inatokana na ubora wa nyakati zake na utukufu wa thawabu ndani yake, kwa sababu kufunga ni miongoni mwa matendo bora kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).
Mwezi wa Allaah Muharram ni mwezi ambao mwaka wa Kiislamu huanza nao, kama ilivyokubaliwa katika zama za khaliyfah aliyeongoka ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Ni miongoni mwa miezi mitukufu ambayo Allaah ameitaja ndani ya Kitabu Chake. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ
”Hakika idadi ya miezi mbele ya Allaah ni kumi na mbili katika hukumu ya Allaah, tangu siku Aliyoumba mbingu na ardhi – kati ya hiyo kuna minne Mitukufu. Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, basi msijidhulumu humo nafsi zenu.”[2]
Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“… mwaka una miezi kumi na mbili, kati yake kuna miezi minne mitukufu: mitatu mfululizo – Dhul-Qa´dah, Dhul-Hijjah na Muharram – na Rajab wa Mudhwar ulioko kati ya Jumaadaa na Sha´baan.”[3]
Kuna maafikiano juu yake.
Allaah ameufungamanisha mwezi huu na nafsi Yake kwa heshima na utukufu, kwa kuwa Allaah (´Azza wa Jall) haambatanishi na nafsi Yake chochote isipokuwa kile kilicho bora kabisa miongoni mwa viumbe, kama vile Nyumba ya Allaah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mfano wake. Umeitwa ”Muharram” kwa ajili ya kusisitiza kuwa ni mwezi uliokatazwa kupigana vita ndani yake, kwa sababu waarabu walikuwa wakichezea hukumu yake – mwaka huu wanaruhusu vita na mwaka mwingine wanakiharamisha. Maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):
فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ
”… basi msijidhulumu humo nafsi zenu.”
Kwa maana ndani ya hiyo miezi mitukufu, kwa sababu dhuluma ndani ya miezi hiyo ni nzito zaidi katika dhambi kuliko katika miezi mingine. Qataadah (Rahimahu Allaah) amesema:
“Hakika dhuluma ndani ya miezi mitukufu ni dhambi kubwa na ina uzito zaidi kuliko dhuluma katika miezi mingine, ingawa dhuluma ni kubwa kwa hali yoyote, lakini Allaah hutukuza atakavyo mambo Yake.”[4]
Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amefanya miezi hii ya mwandamo kuwa ni miadi kwa ajili ya watu, kwa sababu ni alama zinazoonekana waziwazi; kila mtu anaweza kutambua mwanzo na mwisho wake.
[1] Muslim (1163).
[2] 09:36
[3] al-Bukhaariy (4662) na Muslim (1679).
[4] Tafsiyr ya Ibn Kathiyr (4/89-90).
- Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 51-52
- Imechapishwa: 15/05/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket
Related
28. Swawm bora kabisa baada ya Ramadhaan
Ni jambo la kusikitisha kuwa wengi katika waislamu wameacha kutumia tarehe ya Hijriyyah na kuchukua tarehe ya kikristo ya Miladiy ambayo imejengwa juu ya miezi ya kubuni, isiyo na msingi wa Kishari´ah, kiakili wala wa kihisia. Hili linaonyesha udhaifu, kushindwa na kuwafuata wasio waislamu. Miongoni mwa maovu yake ni kuwaunganisha…
In "Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq"
24. Swawm zilizopendekezwa III
7- Kufunga mwezi wa Allaah Muharram. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Swawm bora baada ya Ramadhaan ni mwezi wa Allaah Muharram. Na swalah bora baada ya faradhi ni swalah ya usiku.”[1] 8- Kufunga siku tisa za Dhul-Hijjah. Siku hizi…
In "2. Suala la pili: Swawm iliyopendekezwa"
Ubora wa Muharram ni mwezi wote
Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Swawm bora baada ya Ramadhaan ni mwezi wa Allaah Muharram.” Kunakusudiwa ´Aashuuraa´ - ile siku ya kumi - au mwezi mzima? Jibu: Mwezi mzima. Asipoweza kufunga mwezi wote na akafunga tarehe 10, 09 au 11 ni sawa – Allaah akitaka.
In "Swawm katika Muharram"