Msingi wa dini na uongofu ni kuanza kujifunza ´Aqiydah. Kitu cha kwanza unachotakiwa kuanza kuwafunza watu ni ´Aqiydah. Hii ndio dini ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Usijichoshe nafsi yako ikiwa ´Aqiydah yako si sahihi. Usiwakataze watu kuacha ribaa na uzinzi ikiwa wanafanya shirki. Kwanza unatakiwa kuwakataza shirki ambayo ndio dhambi kubwa ambayo Allaah ameasiwa kwayo. Pindi watu watapokuwa wapwekeshaji ndio utawakataza ribaa, uzinzi na madhambi mengine. Hakuna faida ya kuwakataza madhambi haya pasi na msingi. Endapo wataacha kula ribaa, uzinzi na wizi lakini wakawa wanashirikisha hawafaidiki na kitu. Matendo yao ni bure. Msingi na asili ni Tawhiyd na ´Aqiydah iliosalimika.

Ni lazima kwa walinganizi kwanza kuitilia umuhimu ´Aqiydah. Wako wajinga wanaosema kuwa makafiri pekee ndio wanaotakiwa kulinganiwa katika ´Aqiydah na kwamba waislamu hawana haja ya ´Aqiydah. Ni fikira ya kimakosa. Baadhi ya waislamu wako na upungufu katika ´Aqiydah na hawaijui ´Aqiydah – ilihali wanajiita kuwa ni waislamu. Kwa hivyo tunatakiwa kuanza na waislamu kwanza. Rekebisha ´Aqiydah na msingi wao. Baada ya hapo ndio wende katika mambo mengine, unatakiwa kuanza na wale walio karibu zaidi kisha ndio wende kwa wanaofuata:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ

“Na onya jamaa zako wa karibu.”[1]

Tunawabainishia upotofu ili wajiepushe nao. Isitoshe kuna khatari kwa waislamu kuingia katika shirki na hivyo wakapotea. Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuishilia peke yake kumuomba Mola wake amkinge kuyaabudia masanamu, bali alichelea juu ya nafsi yake kuyaabudia. Hakuitakasa nafsi yake. Kwa hivyo waislamu wanahitaji kulinganiwa katika ´Aqiydah. Baadhi ya waislamu wako na ujinga na wanahitaji kufunzwa. Wengine wako na hoja tata na wanahitaji ubainifu. Wengine wamezungukwa na walinganizi waovu na kwa ajili hiyo wanatakiwa kukabiliwa na kusambaratishwa ili ulinganizi uwe umeanza matokeo salama na sahihi. Ulinganizi wa Tawhiyd sio kwa makafiri peke yao – bali waislamu pia wanahitaji ´Aqiydah na mafunzo ya ´Aqiydah. Waislamu wengi hawaijui ´Aqiydah. Anasema kuwa yuko katika maumbile na dini, lakini endapo utamuuliza swali la ´Aqiydah hajui jawabu. Kwa sababu ni mjinga na mjinga anatakiwa kufunzwa.

[1] 26:214

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 31/07/2024