Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa kwanza – ujuzi wa kumjua Mola

Kukisemwa: “Ni nani Mola Wako?” Jibu: “Mola Wangu ni Allaah ambaye amenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema Zake. Yeye ndiye ninayemwabudu na sina mwabudiwa mwingine asiyekuwa Yeye.”

MAELEZO

Mola – Bi maana ni nani Mola wako aliyekuumba, akakutunuku na akakuruzuku.

Malezi – Ni ibara ya uangalizi ambao malezi ya mlelewa hujengeka juu yake. Maneno ya mtunzi yanaashiria kwamba neno ´Mola` limechukuliwa kutoka katika neno ´malezi`, kwa sababu amesema:

“Mola Wangu ni Allaah ambaye amenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema Zake.”

Allaah amewalea walimwengu wote kwa neema Zake, akawaandaa kwa yale aliyowaumba kwa ajili yake na akawatunuku riziki Yake. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema kuhusu mdahalo kati ya Muusa na Fir´awn:

قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَى قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَى كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَى

Akasema: “Basi nani huyo Mola wenu, ee Muusa?” Akasema: “Mola wetu ni Yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza.” (Twaaha 20 : 49-50)

Kwa hivyo viumbe vyote vimelelewa kwa neema za Allaah (´Azza wa Jall). Neema za Allaah (´Azza wa Jall) kwa viumbe Vyake ni nyingi na haiwezekani kuzidhibiti. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا

“Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuzidhibiti.” (an-Nahl 16 : 18)

Allaah ndiye ambaye amekuumba, akakuandaa, akakutunuku na akakuruzuku. Kwa hiyo Yeye pekee ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa.

Yeye ndiye ninayemwabudu… – Yeye ndiye ninayemwabudu na kujisalimisha Kwake hali ya kumnyenyekea, kumpenda na kumtukuza. Ninafanya yale aliyoniamrisha na kuacha yale aliyonikataza. Sina mwingine ninayemwabudu asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mungu wa haki isipokuwa Mimi – hivyo basi Niabuduni.” (al-Anbiyaa´ 21 : 25)

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.” (al-Bayyinah 98 : 05)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 20/05/2020