Kuna sampuli mbili za kutofautiana:

1 – Kutofautiana katika ´Aqiydah. Tofauti kama hii haijuzu kabisa kwa sababu inapelekea kugombana, adui, chuki na mgawanyiko. Kwa hivyo ni wajibu kwa waislamu wawe na ´Aqiydah moja, Tawhiyd, kimaneno, kimatendo na kiimani. ´Aqiydah ni jambo linaloweza kutolewa ndani ya Qur-aan na Sunnah na hakuna nafasi ya kufanya Ijtihaad. Mambo yakishakuwa hivo basi hapana nafasi yoyote ya kufarikiana. ´Aqiydah inachukuliwa kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah, na si kutoka katika maono na Ijtihaad. Kutofautiana katika ´Aqiydah kunapelekea kugombana, kuchukiana na kukatana, kama ilivyowatokea Jahmiyyah, Mu´tazilah, Ashaa´irah na mapote mengine ya upotofu, aliyoyaelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Ummah huu utafarikiana makundi sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wataofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah wangu.”[1]

Hakuna yatayowakusanya watu isipokuwa kufuata yale ambayo yalikuwa yakifuatwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake.

2 – Kutofautiana katika Ijtihaad za ki-Fiqh. Tofauti kama hii haipelekei katika uadui kwa sababu inatokana na kuziangalia dalili kutegemea na mitazamo ya watu, jambo ambalo watu wanatofautiana kwalo. Hawalingani katika jambo hilo. Wanatofautiana katika nguvu ya uchimbaji na kiwango cha elimu. Tofauti hii ikiwa haikuambatanishwa na ushabiki, basi haipelekei katika uadui. Maswahabah walikuwa wakitofautiana katika mambo ya ki-Fiqh na hakutokei kati yao uadui. Waliendelea kubaki ndugu. Vivyo hivyo walitofautiana wema waliotangulia na maimamu wanne. Wakati mmoja atashikilia kishabiki maoni fulani, basi hapo ndipo itapelekea katika uadui. Muislamu anatakiwa kuchukua tu yale maoni yanayoafikiana na Qur-aan na Sunnah. Allaah (Subhaanah) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

”Jambo lolote lile mlilokhitilafiana kwalo, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[3]

Wakati wa kutofautiana mtu anatakiwa kurudi katika Qur-aan na Sunnah na kufanyia kazi yale yenye nguvu zaidi kwa mujibu wa dalili.

[1] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[2] 4:59

[3] 42:10

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 255-256
  • Imechapishwa: 07/05/2025