Haafidhw Abu Nu´aym al-Aswbahaaniy amesema:

“Mfumo wetu ni uleule mfumo wa Salaf wa kufuata Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya ummah… Allaah ametengana na viumbe Vyake na viumbe wametengana Naye. Hakukita ndani yao, hachangamani nao. Yeye amelingana juu ya ´Arshi Yake juu ya mbingu Zake mbali na ardhi Yake.”

Imaam Abu Zakariyyaa Yahyaa bin ´Ammaar as-Sijistaaniy amesema katika kijitabu chake:

”Hatusemi kama wanavosema Jahmiyyah, kwamba Yeye huingia katika sehemu na kwamba amechanganyikana na kila kitu au kwamba hatujui Yuko wapi. Bali tunasema kuwa Yeye yuko juu ya ´Arshi kwa dhati Yake na kwamba ujuzi Wake umekizungukaa kila kitu. Ujuzi, usikizi, uoni na uwezo Wake umekizunguka kila kitu. Hiyo ndio maana ya maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye yupamoja nanyi popote mlipo.”[1]

Hiki ndicho tulichokisema ya kwamba sehemu haziko tupu kutokana na ujuzi na uwezo Wake na kwamba Yeye huzifikia kwa kusikia na kuona Kwake. Sambamba na hilo Yeye yuko juu ya ´Arshi kwa dhati Yake. Hivo ndivo alivyosema Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Imaam Abu ´Uthmaan as-Swaabuuniy amesema:

”Ahl-ul-Hadiyth wanaitakidi na kushuhudia ya kwamba Allaah (Subhaanah) yuko juu ya mbingu ya saba na amelingana juu ya ´Arshi Yake, kama Alivotamka Mwenyewe ndani ya Kitabu Chake… Wanazuoni wa ummah na maimamu wa Salaf (Rahimahumu Allaah) hawakuwahi kukhitilafiana juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi Yake na kwamba ´Arshi Yake iko juu ya mbingu Zake. Wanamthibitishia yale ambayo Allaah (Ta´ala) amejithibitishia Mwenyewe…. Imamu wetu Abu ´Abdillaah Muhammad bin Idriys ash-Shaafiy´iy (Rahimahu Allaah) amesema ndani ya kitabu chake[2] alichozungumza kwa upana juu ya suala la kumwacha huru mtumwa wa kiislamu katika kafara:

”Kutokana na Hadiyth ya Mu´aawiyah bin al-Hakam haijuzu kulipa kafara kwa mtumwa asiyekuwa muumini. Alitaka kumwacha huru kijakazi mweusi na akamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kumwacha huru. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa mtihani na kumuuliza: ”Mimi ni nani?” Akamwashiria yeye na mbinguni.” Bi maana, wewe ni Mtume wa Allaah ambaye yuko juu ya mbingu. Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”[3]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamthibitishia Uislamu na imani yake wakati alipotambua kuwa Mola wake yuko juu ya mbingu na akamtambua kwa sifa ya kuwa na ujuu na kuwa juu.”[4]

Faqiyh Abul-Fath Sulaym bin Ayyuub ar-Raaziy, swahiba yake Shaykh Abu Haamid al-Isfaraayiyniy, amesema katika tafsiri yake ya Qur-aan katika mnasaba wa maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[5]

Abu ´Ubaydah amesema:

”Kwa maana ameinuka juu.”

Wengine wamesema:

”Kwa maana amethibiti.”

Qataadah amesema katika mnasaba wa maneno Yake (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Yeye Ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi.”[6]

”Kwa maana katika siku ya saba.”

Imaam Abu ´Amr ad-Daaniy amesema:

Amemzungumzisha Muusa mja wake maneno ya kweli

Hakuacha kuwa ni Mwenye kusimamia na Mwenye hekima

Maneno Yake na kauli Yake ni ya milele

Na Yuko juu ya juu ya ´Arshi Yake tukufu

Na maoni sahihi juu ya kitabu Chake

ni kwamba ni maneno Yake  yaliyosushwa

kwa Mtume na Nabii Wake mkweli

si kiumbe wala hayakuumbwa

Kusema kuwa ni kiumbe au kutengenezwa ni kuritadi[7]

[1] 57:4

[2] ´Allaamah Rabiy´ al-Madkhaliy amesema:

”Bi maana kwenye kitabu chake ”al-Umm”.” (Sharh ´Aqiydat-is-Salaf wa Aswhab-il-Hadiyth, uk. 99)

[3] Muslim (537), Abu Daawuud (930), an-Nasaa’iy (3/13), Maalik (2/776), Ibn Abiy ´Aaswim (479), al-Bayhaqiy, uk. 422, Ahmad (5/447), Abu Daawuud at-Twayaalisiy (1105) na Ibn Khuzaymah katika ”at-Tawhiyd”, uk. 121.

[4] ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhhaab-il-Hadiyth, uk. 188.

[5] 20:5

[6] 57:4

[7] ´Uquud Ahl-is-Sunnah, uk. 30-31

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 80-82
  • Imechapishwa: 29/12/2025