23. Alipangusa soksi kivyake, na viatu kivyake

Vilevile an-Nawawiy amesema:

”al-Bayhaqiy amesimulia kutoka kwa an-Naysabuuriy kwamba aliifasiri Hadiyth hiyo kuwa ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipangusa juu ya jozi za soksi zilizo na viatu chini yake, si soksi peke yake na kiatu peke yake, kana kwamba alisema kwamba alipangusa juu ya soksi zake zilizo na viatu chini yake. Basi kwa hilo anamaanisha aliyoyasema al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan” yake, ambapo alisimulia hilo kisha akasema baada yake: “Nimekuta kwa Anas masimulizi yanayoonyesha hilo”, kisha akapokea kutoka kwake kwamba alipangusa juu ya soksi ambazo chini yake zilikuwa ngozi na juu yake zilikuwa hariri.”[1]

Hilo likapingwa na ´Allaamah ‘Alaa-ud-Diyn al-Mardiniy ”al-Jawhar an-Naqiy” kwa kusema:

”Hadiyth hii – yaani Hadiyth ya al-Mughiyrah – imekuja kwa kuunganisha viatu na soksi kwa herufi ya “na”, nayo huashiria utofauti. Kwa hivyo tamko lake linapingana na tafsiri hii. Kitendo cha Anas cha kupangusa juu ya soksi zilizo na viatu chini yake hakilazimishi kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) naye alifanya hivyo. Kitendo cha Anas hakifahamishi kufasiri Hadiyth kwa namna ambayo tamko lake halionyeshi hivo.”

Ibn-ul-Hammaam akasema katika ”Fath-ul-Qadiyr” wakati alipokuwa akiraddi tafsiri hii:

”Kuifungia ruhusa kuwepo kwa kiatu wakati huo ni kuibana dalili – yaani Hadiyth – na kuipunguzia maana yake bila sababu.”

Kwa maana kwamba bila chochote kinachoihitaji hilo, si kutoka katika tamko lake wala kutoka katika maana yake, kwa kuwa dhahiri yake ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipangusa juu ya soksi na juu ya viatu, kila kimoja peke yake.

[1] Cheni ya wapokezi ya al-Bayhaqiy ni nzuri na dalili ya al-Maardiyniy ni yenye nguvu sana.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 08/04/2026