Kuna uchawi sampuli mbili:

1 – Uchawi wa kikweli. Uchawi wa kweli ni ule unaoathiri mwili wa aliyefanyiwa uchawi na hivyo akawa mgonjwa, ukaathiri akili yake au ukamuua kabisa. Haya ni matendo ya kishaytwaan.

2 – Uchawi wa mazingaombwe. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ

“… zikaonekana kwake  [yeye Muusa] kutokana na uchawi wao zinakwenda mbio.”[1]

Huu ndio ule uchawi unaoitwa ´kiini macho` ambapo wanafanya kitu mbele ya watu ilihali hakuna ukweli wowote. Anawaonyesha eti anajipiga upanga, anakula mikuki, moto au vioo, anaingia ndani ya moto, magari yanatembea juu yake, analala juu ya misumari, anavuta gari kwa nywele zake au analeta karatasi za kawaida na kuwaonyesha watu kuwa eti ni pesa, pindi unapoondoka uchawi basi noti zinarudi kuwa karatasi za kawaida. Matendo kama haya hufanywa na matapeli. Mifano mingine ni kuwa wanafanya mbawakawa kuonekana kama kondoo au kutembea juu ya kamba nyembamba. Haya ya mwisho ndio yale huitwa kuwa ni sarakasi au wachekeshaji. Yote haya ni uwongo na kuwahadaa watu na ni kuyaroga macho ya watu. Aidha ni uchawi wa kiini macho. Unapoisha nguvu uchawi huu basi mambo yanarudi kawaida kama yalivyokuwa. Kwa hivyo ni lazima kwetu tusidanganyike nao, tusiwasadikishe na tusiwaache wakamakinika kwa watoto wetu wala katika miji yetu.

[1] 20:66

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 249-250
  • Imechapishwa: 06/05/2025