Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

168 – Hatumsadikishi kuhani, mpiga ramli wala yeyote anayedai kitu kinachoenda kinyume na Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Ummah.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu amekwishatangulia kutaja karama na vigezo vyake, akathibitisha kuwa ni haki lakini kwamba haijuzu kuzitegemea. Aidha kwamba mawalii hawana haki ya kuabudiwa pamoja na Allaah, kama wanavosema waabudia makaburi na makhurafi ambao wanawategemea mawalii na waja wema wanaofanya mambo haya yasiyokuwa ya kawaida.

Hapa mtunzi (Rahimahu Allaah) anatofautisha kati ya karama, ukuhani, upigaji ramli, uchawi na mambo ya unajimu. Haya yanayofanywa na makuhani na wapiga ramli ni mambo yasiyokuwa ya kawaida ya kishaytwaan, wameyamairi na kujifunza nayo kwa sababu ya kujikurubisha kwao kwa mashaytwaan. Matokeo yake watu wa kawaida na wajinga wakadhani kuwa mambo hayo ni karama za kweli, zinazotokana na urafiki wao na Allaah. Hili ni kosa. Hayo ni katika matendo ya mashaytwaan, kwa sababu ya kule kuwanyenyekea kwao na kukubaliana nao katika shirki zao. Wachawi hawakuweza kufanya uchawi isipokuwa ni kwa sababu ya kuwanyenyekea kwao mashaytwaan. Uchawi ni katika matendo ya shaytwaan na ni kumkufuru Allaah. Kwa ajili hiyo mtu asighurike nao. Wanayaita matendo yao kuwa ni karama, mazoezi au sarakasi, na wanahudhuria katika mikusanyiko ya watu na matamasha. Wanafanya uchawi mbele ya watu kwa kutumia jina la mazoezi, kuwapotosha watu na kula mali za watu kutokana na uchawi huu. Kwa ajili hiyo ni lazima kuwazindua watu hawa, kuwachukia na kuwazingatia kuwa ni maadui, kwa sababu ni maadui wa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 248-249
  • Imechapishwa: 30/04/2025