22. Kumwomba Allaah kunajulisha kumnyenyekea Allaah

Miongoni mwa ´ibaadah zinazofahamisha kumdhalilikia na kumnyenyekea Allaah  (´Azza wa Jall) ni du´aa. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

“Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye hawapendi wenye kuvuka mipaka.”[1]

وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri.”[2]

Miongoni mwa vitu vinavyojulisha unyenyekevu katika du´aa ni kule kunyanyua juu mikono. Imesihi kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alinyanyua mikono yake wakati wa kuomba du´aa katika maeneo mengi, ambapo kubwa zaidi ni pale wakati wa kuomba du´aa ya kunyesheleza mvua. Wakati alipokuwa anaomba alikuwa akinyanyua mikono yake mpaka kunaonekana weupe wa makwapa yake[3]. Vivyo hivyo alikuwa akijitahidi kuinua mikono yake mchana wa ‘Arafah. Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesimulia:

“Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) akiomba du´aa ´Arafah huku mikono yake ikiwa juu ya kifua chake, kama maskini anayeomba chakula.”[4]

Ameipokea at-Twabaraaniy.

Watu waliokuwa wakimcha Allaah walikuwa wakikesha usiku huku wakiwa tuli hali ya kuinamisha vichwa vyao na wakinyoosha mikono yao kama ombaomba. Ni miongoni mwa dalili kubwa za kujidhalilisha, utii na uhitaji.

[1] 07:55

[2] 21:90

[3] al-Bukhaariy (1030-1031) na Muslim (895-897).

[4] at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw” (2892-2893). al-Haythamiy amesema:

“Katika cheni ya wapokezi kuna al-Husayn bin ´Abdillaah bin ´Ubaydillaah, ambaye alikuwa mnyonge.” (Majma´-uz-Zawaa-id (10/168))

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 24/11/2025