Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:
155 – Hatuchupi mipaka katika kumpenda yeyote katika wao, wala hatujitengi mbali na yeyote katika wao.
MAELEZO
Hatuchupi mipaka katika kumpenda yeyote katika wao kama walivofanya Raafidhwah katika kumpenda ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kama wanavodai. Vinginevyo udhahiri ni kwamba hawawapendi na wala hawawapendi Maswahabah wote kwa jumla. Wamechupa mipaka kwake mpaka baadhi yao wakafikia kusema eti ´Aliy ndiye Allaah. ´Aqiydah hiyo ilizuka katika zama za ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), ambapo akawachimbia mashimo na kuwachoma moto kwa sababu ya ghera kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall).
Kupetuka mipaka kumekatazwa, ni mamoja kwa Maswahabah au kwa mwengine. Allaah (Subhaanah) amesema:
قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ غَيْرَ الْحَقِّ
“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Msichupe mipaka katika dini yenu bila ya haki.”[1]
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Tahadharini kutokana na kuchupa mipaka. Hakika hapana vyengine kilichowaangamiza waliokuwa kabla yenu ni kuchupa mipaka.”[2]
Sisi tunawapenda Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini hatuchupi mipaka juu yao mpaka tukawafanya kuwa washirika wa Allaah na tukawaomba badala ya Allaah, kama wanavofanya Raafidhwah na waabudia makaburi. Huku sio kuwapenda Maswahabah. Kuwapenda ni kwa kuwapenda, kuwaigiliza na kuwatakia radhi.
Wala hatujitengi mbali na Maswahabah. Hapa kuna ishara kwa Raafidhwah, ambao wanajiweka mbali kutokana na Maswahabah, khaswakhaswa Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anhum). Bali wanawakufurisha wengi katika Maswahabah, jambo ambalo ni katika kuzembea. Kwa hivyo hatuzembei katika kuwapenda, kwa sababu kuzembea ni kule kuacha kuwapenda.
[1]5:77
[2]an-Nasaa’iy (3057), Ibn Maajah (3029), Ahmad (1851) na Ibn Hibbaan. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (2455).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 231
- Imechapishwa: 27/04/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)