21. Tofauti kati ya mpwekeshaji na mshirikina

al-Haarith al-Ash’ariy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) alimwamuru Yahyaa bin Zakariyyaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno matano ayatende na awaamrishe nayo wana wa israaiyl wayatende na kwamba alikuwa karibu achelewe kuyatekeleza. Ndipo ´Iysaa (´alayhis-salaam) akamwambia: ”Hakika Allaah amekuamrisha kwa maneno matano uyatende na uwaamrishe wana wa israaiyl wayatende. Ama utawaamrisha au mimi nitawaamrisha.” Yahyaa akasema: “Ninachelea kwamba ukinitangulia kwa hayo nitateremshiwa adhabu na niadhibiwe.” Basi Yahyaa akawakusanya watu katika Yerusalemu, msikiti ukajaa naye akaketi juu ya jukwaa na kusema: “Hakika Allaah ameniamrisha kwa maneno matano niyatende na niwaamrishe myatende. La kwanza ni kwamba mumuabudu Allaah na wala msimshirikishe na chochote. Hakika mfano wa anayemshirikisha Allaah ni kama mtu aliyenunua mtumwa kwa mali yake yote, dhahabu au fedha ambapo akamwambia: ”Hii ni nyumba yangu na hii ni kazi yangu. Fanya kazi na nirejeshee.” Basi akaanza kufanya kazi, lakini akimrejeshea mwingine asiye bwana wake. Je, ni nani miongoni mwenu anayependezwa mtumwa wake kuwa hivyo?

Hakika Allaah amewaamrisha swalah. Mnaposwali msiangalie pembeni, kwani Allaah huuelekeza uso Wake kwa uso wa mja Wake katika swalah yake muda w akuwa hajaangalia pembeni.

Amewaamrisha kufunga pia, kwani mfano wa hilo ni kama mtu aliye ndani ya kundi, naye ana harufu nzuri ya mski ambapo wote wanapendezwa na harufu yake. Hakika harufu ya mfungaji ni bora zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya mski.

Amewaamrisha vilevile kutoa swadaqah. Mfano wake ni kama mtu aliyetekwa na adui. Wakamfunga mikono yake kwenye shingo yake na wakamleta wamkate shingo yake. Akasema: ”Nitakomboa nafsi yangu kwa kidogo au kingi.” Matokeo yake akajikomboa nao.

Amewaamrisha pia kumdhukuru Allaah. Mfano wake ni kama mtu aliyetafutwa na adui kwa kasi mpaka akafikia ngome madhubuti, basi akajikinga humo nao. Hali kadhalika mja hajilindi dhidi ya shaytwaan isipokuwa kwa kumtaja Allaah (Ta´ala).”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

”Nami nawaamrisheni kwa maneno matano ambayo Allaah ameniamrisha; kusikia, kutii, jihaad, kuhajiri na kushikamana na mkusanyiko. Hakika anayefarikiana na mkusanyiko kiasi cha shibri moja, basi amevua kongwa ya Uislamu kutoka shingoni mwake, isipokuwa atakaporejea. Yeyote anayejigamba kwa wito wa kipindi kabla ya kuja Uislamu, basi ni miongoni mwa watu wa Jahannam.” Bwana mmoja akasema: “Ee Mtume wa Allaah, hata akaswali na kufunga?” Akasema: “Hata kama ataswali na kufunga. Lakini waiteni kwa wito wa Allaah aliyekuiteni ”waislamu na ”waumini”.”[1]

Ameipokea Imaam Ahmad (Radhiya Allaahu ´anh) na at-Tirmidhiy, ambaye amesema kuwa  Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametaja katika Hadiyth hii adhimu yenye cheo, ambayo inamstahiki kila muislamu kuifahamu na kuitafakari yale yanayomkinga mtu na shaytwaan na yale yanayomletea mja ushindi na uokozi katika dunia na Aakhirah yake. Ametaja mfano wa mpwekeshaji na mshirikina. Mpwekeshaj ni kama aliyefanya kazi kwa ajili ya bwana wake ndani ya nyumba ya bwana wake na akamrejeshea bwana wake kile alichotumika nacho. Mshirikina ni kama mtu ambaye bwana wake alimfanyisha kazi ndani ya nyumba yake, lakini akafanya kazi na akamrejeshea mazao yake kwa mtu mwingine asiye bwana wake. Hali kadhalika mshirikina anafanya kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah ndani ya nyumba ya Allaah na anajikurubisha kwa adui wa Allaah kwa neema za Allaah. Ni jambo linalojulikana kwamba mja miongoni mwa wanaadamu lau mtumwa wake angekuwa kama huyo, basi angekuwa ni mwenye kuchukiwa zaidi kwake, ndiye angekuwa ni kitu cha ghadhabu zaidi kwake na kingetupwa mbali zaidi, ilihali yeye ni kiumbe kama yeye, wote wako katika neema ya mwingine. Basi tusemeje juu ya Mola wa walimwengu wote ambaye hakuna neema yoyote kwa mja isipokuwa ni yenye kutoka Kwake peke Yake asiye na mshirika yeyote, hakuna anayekuja na mema isipokuwa Yeye na wala hakuna anayeondoa mabaya isipokuwa Yeye? Yeye peke Yake ndiye aliyemuumba mja wake, akamrehemu, akamtengea mambo yake, akamruzuku, akamponya na akamtimizia mahitajio yake. Basi vipi inafaa kwa mja pamoja na hayo yote kumshirikisha Naye mwingine katika mapenzi, khofu, matumaini, kuapiza, nadhiri na miamala ambapo akampenda mwingine kama anavyompenda Yeye au zaidi, akamwogopa mwingine na kumtarajia kama anavyotarajiwa Yeye au zaidi? Dalili za hali zao, bali hata maneno na vitendo vyao, vinathibitisha kuwa wanayapenda masanamu yao miongoni mwa waliohai na waliokufa, wanawaogopa, wanawatarajia, wanatafuta radhi zao na wanakimbia ghadhabu zao zaidi kuliko wanavyompenda Allaah, wanavyomwogopa, wanavyomtazamia na wanavyokimbia ghadhabu Zake.

[1] Ahmad (5/849-850) na at-Tirmidhiy (2863).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 37-39
  • Imechapishwa: 04/08/2025