88 – Abu ´Abdillaah Muhammad bin ´Aliy bin ´Abdillaah as-Suuriy alinisomea:

Ni asubuhi sijarauka

kwa nia moja kabisa na kwa kunyamaza nitafute elimu

pasi na kufanyia matendo chochote

Ikiwa mwanafunzi haitendei kazi elimu

anakuwa ni mja aliyekula khasara

Elimu inamnufaisha yule ambaye

anaifanyia kazi na akawa anamcha Allaah

89 – Abul-Faraj ´Abdus-Salaam bin ´Abdil-Wahhaab al-Qurashiy ametukhabarisha: Sulaymaan bin Ahmad bin Ayyuub at-Twabaraaniy ametuzindua: Muttwalib bin Shu´ayb al-Azdiy ametuhadithia: ´Abdullaah bin Swaalih ametuhadithia: al-Layth amenihadithia… at-Twabaraaniy amesema: Abuz-Zanbaa´ Rawh bin al-Faraj ametuhadithia: Yahyaa bin Bukayr ametuhadithia: al-Layth ametuhadithia, kutoka kwa Ibraahiym bin Abiy ´Ulayyah, kutoka kwa al-Waliyd bin ´Abdir-Rahmaan al-Jurashiy, kutoka kwa Jubayr bin Nufayr: ´Awf bin Maalik al-Ashja´iy amenihadithia:

”Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitazama juu mbinguni akasema: ”Umefika wakati wa kuenuliwa elimu.” Bwana mmoja katika Wanusuraji, kwa jina la Ziyaad bin Labiyb, akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Itainuliwa elimu ilihali imekwishathibiti na kueleweka na nyoyo?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Nilikuwa nafikiri wewe ndiye mjuzi zaidi katika watu wa Madiynah.” Kisha akataja upotofu wa mayahudi na manaswara licha ya Kitabu cha Allaah walichonacho.  Baadaye nikakutana na Shaddaad bin Aws ambapo nikamweleza Hadiyth ya ´Awf bin Maalik. Akasema: ”´Awf amesema kweli. Je, nisikujuze kitu cha kwanza katika hayo kitachonyanyuliwa?” Nikasema: ”Ndio.” Akasema: ”Unyenyekevu. Hutomuona yeyote ambaye ananyenyekea.”[1]

90 – Abu ´Abdillaah Ahmad bin Muhammad bin ´Abdillaah al-Kaatib ametuzindua: Abu Muslim ´Abdur-Rahmaan bin Muhammad bin ´Abdillaah bin Mihraan ametuzindua: Nilimsomea Abu Ja´far Muhammad bin Ahmad bin Muhammad as-Subahiy: Abu Rajaa’ Muhammad bin Hamduuyah bin Muusa ametuhadithia: Ahmad bin Jamiyl ametuhadithia: Hafsw bin Humayd ametukhabarisha, kutoka kwa Ibn-ul-Mubaarak, ambaye amesema:

”Alikuwepo bwana mmoja mwenye mali ambaye hamsikii mwanachuoni isipokuwa atamwendea ili asome kutoka kwake. Wakati mmoja akasikia kuna mwanachuoni mahali fulani, akapanda safina na ndani yake alikuwepo mwanamke. Mwanamke yule akasema: ”Una nini wewe?” Akasema: ”Mimi nina shauku ya kupenda elimu. Nimesikia kuwa sehemu fulani kuna mwanachuoni, hivyo niko njiani namwendea.” Mwanamke yule akasema: ”Kila ambavyo inazidi elimu yako ndivo unavofanya matendo kwa wingi au unajizidishia tu elimu na matendo yamesimama palepale?” Bwana yule akazindukana, akarejea na kuanza kutenda zaidi.”

91 – al-Qadhwiy Abul-´Alaa’ Muhammad bin ´Aliy al-Waasitwiy ametukhabarisha: Abul-Fath Muhammad bin al-Husayn al-Mawsiliy ametukhabarisha: ´Abdullaah bin ´Aliy al-´Umariy ametuhadithia: al-Fath bin Shakhraf ametuhadithia: ´Abdullaah bin Khubayq ametuhadithia: ´Abdullaah bin as-Sindiy ametuhadithia, kutoka kwa Ibraahiym bin Ad-ham, ambaye amesema:

”Alitoka bwana momoja kwa ajili ya kutafuta elimu ambapo akakutana na jiwe njiani. Jiwe hilo lilikuwa limefanyiwa nakshi: ”Nigeuze, utakuja kuona maajabu na kupata mazingatio!” Akaligauza jiwe hilo na lilikuwa limeandikwa: ”wewe hukifanyii kazi kile unachojifunza. Ni vipi unatafuta usichokifanyia kazi?” Bwana yule akarejea.”

[1] Swahiyh. Ameipokea Ahmad na al-Haakim, ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikina naye. Cheni ya wapokezi ni kwa mujibu wa sharti za Muslim.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy al-Khatwiyb al-Baghdaadiy (afk. 463)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iqtidhwaa’-ul-´Ilm al-´Amal, uk. 57-60
  • Imechapishwa: 13/05/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy