Kwa mnasaba wa Aayah hii tukufu napenda kusema kwamba wakati mwingine Qur-aan tukufu inahadithia khabari kwa neno “sema”. Kila jambo lililoelezwa kwa neno hili maana yake ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amelipa umuhimu maalum kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrishwa kuitamka Qur-aan nzima:

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ

“Ee Mtume! Fikisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako.”[1]

Lakini khabari hii ambayo imekuja kwa neno hili “sema” imetiliwa umuhimu maalum. Khabari hiyo imestahiki kuja kwa aina ya ubalighisho kwa njia maalum. Ni kama mfano wa Aayah tuliyoitaja na mfano wake katika hukumu mbalimbali:

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ

“Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao.”[2]

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao.”[3]

Zipo zengine nyingi mfano wake ndani ya Qur-aan.

Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajui mambo yaliyofichikana isipokuwa yale aliyofunuliwa na Allaah na wala hamiliki juu ya nafsi yake wala juu ya mwengine manufaa wala madhara:

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا

”Sema: ”Hakika mimi similiki juu yenu dhara na wala uongofu.”[4]

قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا

“Sema: “Hakika hakuna yeyote awezaye kunilinda na Allaah na wala sitoweza kupata mahali pa kukimbilia pasi Naye.”[5]

[1] 05:67

[2] 24:30

[3] 24:31

[4] 72:21

[5] 72:22

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 32
  • Imechapishwa: 19/08/2019