Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa Allaah (Ta´ala) ana macho mawili anayoona kwayo. Ni ya kikweli kwa njia inayolingana Naye. Ni katika sifa za kidhati zilizothibiti kwa Qur-aan na Sunnah. Kuhusu Qur-aan, Allaah (Ta´ala) amesema:

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا

”Inatembea chini ya macho Yetu.”[1]

Ama Sunnah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Mola Wetu (Tabaarak wa Ta´ala) si chongo.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anakuangalieni pindi mnapokuwa katika hali ngumu na mmekata tamaa.”[3]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pazia Yake ni nuru. Lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila kile ambacho anakiona katika viumbe Wake.”[4]

Kwa hivyo ni macho mawili ya kihakika na hayafanani na macho ya viumbe. Si sahihi kukengeusha maana yake kwamba ni elimu na maono kwa sababu zifuatazo:

1-  Ni kuondosha maana ya kihakika kwenda katika majazi pasi na dalili.

2- Maandiko yana maana inayopingana na tafsiri kama hiyo. Kwa mfano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anakuangalieni.”

“Pazia Yake ni nuru. Lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila kile ambacho anakiona katika viumbe Wake.”

“Hakika Mola Wetu (Tabaarak wa Ta´ala) si chongo.”

[1] 54:14

[2] al-Bukhaariy (3439) na Muslim (169).

[3] Ahmad (4/11), Ibn Maajah (181) na Ibn Abiy ´Aaswim (554).

[4] Muslim (179).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 58
  • Imechapishwa: 01/05/2020