19. Kutoka kwa Ibn Surayj kwenda kwa al-Khattwaabiy

95 – Imaam Ibn Surayj amesema:

”Ni haramu juu ya akili kumfananisha Allaah, mawazo kumuwekea mpaka na busara kumsifu isipokuwa yale aliyojisifu Mwenyewe ndani ya Kitabu Chake au kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Imesihi kutoka kwa Ahl-us-Sunnah wote mpaka hii leo ya kwamba Aayah na maelezo yote ya kweli kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni lazima kwa muislamu kuyaamini yote kama yalivyopokelewa na atambue kuwa ni Bid´ah kuuliza maana yake na ni kufuru na uzandiki kujibu. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[1]

الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[2]

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

“… na takapokuja Mola wako na Malaika safu kwa safu.”[3]

Na mfano wake ambayo yametamkwa na Qur-aan kama vile ujuu, nafsi, mikono miwili, kusikia, kuona, maneno, macho, kuonekana, matakwa, kuridhia, kukasirika, mapenzi, kusimamia, ukaribu, umbali, kuchukia na hayaa… na zingine zote kuhusu sifa zenye kutatiza zilizosihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Aayah za Qur-aan mfano wake ya kwamba tunazikubali na wala hatuzirudishi wala hatuzipindishi maana na kuzifananisha, kama wanavofanya Mushabbihah wala kuzifasiri kwa lugha isiyokuwa ya kiarabu.”

Alifariki mwaka wa 306 na alikuwa akitangulizwa mbele kabla ya Shaafi´iyyah wote, hata al-Muzaniy. Alitunga tungo 400.

96 – Abu Ja´far Muhammad bin Jariyr at-Twabariy amesema katika kitabu chake ”at-Tabswiyr fiy Ma´aalim-id-Diyn”:

”Mfano wa zile sifa ambazo zinaweza kutambulika kwa Qur-aan na Sunnah peke yake ni kama pale ambapo (´Azza wa Jall) anaeleza kuwa Yeye ni…

1 – … Mwenye kusikia na kuona…

2 – … kwamba ana mikono miwili Aliposema:

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali mikono Yake imekunjuliwa.”[4]

3 – … kwamba ana uso pale Aliposema:

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ

“Na utabakia uso wa Mola Wako.”[5]

4 – … kwamba ana mguu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”… mpaka pale ambapo Mola wako ataweka mguu Wake juu yake.”

5 – … kwamba anacheka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”… atakutana na Allaah hali ya kuwa anamcheka.”

6 – … kwamba anashuka katika mbingu ya chini, kama alivyoeleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

7 – … kwamba ana vidole. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakuna moyo wowote isipokuwa uko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa rehema.”

Maana hizi na mfano wake nilizotaja ambazo Allaah amejisifu Mwenyewe na pia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haziwezi kuthibitishwa kwa kufikiria wala kutafakari. Wala hatukufurishi kwa kuwa mjinga kwazo mpaka asimamikiwe na hoja.”[6]

Muhammad bin Jariyr alifariki mwaka wa 310. Alikuwa ni mmoja katika wanazuoni wenye utambuzi uliotimia katika Qur-aan, Hadiyth, Fiqh, kiarabu na historia. Alikuwa akihukumu kwa maoni yake na akifanya maoni yake ndio marejeo. Alikusanya elimu ambazo hakuna yeyote katika wakati wake alifanya hivo. Imamu wa maimamu Ibn Khuzaymah amesema:

”Simjui yeyote juu ya uso wa ardhi ambaye ni mtambuzi zaidi kuliko Muhammad bin Jariyr.”

Imaam Abu Haamid al-Isfaraayiyniy amesema:

”Ikiwa mtu atasafiri kwenda mpaka China ili aweze kupata tafsiri ya Qur-aan ya Muhammad bin Jariyr, asingekuwa amefanya kazi kubwa.”

97 – Imaam Abu Sulaymaan al-Khattwaabiy amesema:

”´Aqiydah ya Salaf juu ya Aayah za sifa na Hadiyth zake ni kuzipitisha kwa udhahiri wake na kuzikanushia namna na ufanano. Kuna kundi limezikanusha ambapo wakabatilisha yale aliyoyathibitisha Allaah. Kundi lingine wakazihakikisha sana mpaka wakaanza kuzifananisha na kuzifanyia namna. Njia ya kati na kati ndio inayotakiwa kufuatwa. Dini ya Allaah (Ta´ala) iko baina ya upetukaji na uzembeaji.”

Kanuni ni kwamba kuzungumzia sifa ni sehemu ya kuzungumzia dhati, yote hayo mawili yanatakiwa kutunzwa sawasawa. Ikiwa ni jambo linalofahamika ya kwamba kumthibitisha Muumba (Subhaanahu wa Ta´ala) inahusiana na kuthibitisha uwepo Wake na si kuthibitisha namna Yake, basi vivyo hivyo kuthibitisha sifa Zake inahusiana na kuthibitisha uwepo Wake na si kuthibitisha namna yake.”

Pindi kwa mfano tunasema mkono, usikiaji au uonaji, hivyo inahusiana na sifa ambazo Allaah amejithibitishia nazo Mwenyewe. Hatusemi kuwa maana ya mkono ni nguvu na neema. Wala hatusemi kuwa usikizi na uoni maana yake ni ujuzi. Na wala hatusemi kuwa ni viungo vya mwili. Wala hatuzifananishi na mikono, masikizi na maono ambayo ni viungo kikweli. Sababu ya kwamba ni lazima kuzithibitisha sifa hizi ni kwa kuwa zimetajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Aidha ni lazima kuzikanushia ufanano kwa sababu Allaah hafanani na chochote. Huo ndio ulikuwa msimamo wa Salaf juu ya Hadiyth zinazozungumzia sifa.”

Haya yote ni maneno yamesemwa na al-Khattwaabiy katika kitabu chake ”al-Ghunyah ´an-il-Kalaam wa Ahlih”. Alikuwa ni imamu mkubwa na bingwa katika Hadiyth, Fiqh na maoni ya wanazuoni. Ameandika kitabu ”Ma´aalim-us-Sunan” na ”Kitaab-ul-Ghariyb”. Alifariki mwaka wa 370.

[1] 2:210

[2] 20:5

[3] 89:22

[4] 05:64

[5]55:27

[6] Uk. 132

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 90-94
  • Imechapishwa: 05/06/2024