19. Hadiyth ina uzito zaidi kuliko maoni ya wanazuoni wengi

Imaam an-Nawawiy amesema katika ”Sharh-ul-Muhadhdhab”:

”Maswahiba zetu wametoa hoja[1] kwamba haiwezekani kuendelea kutembea juu yake, hivyo haikujuzu kama kitambaa… Majibu juu ya Hadiyth ya al-Mughiyrah ni kwa njia nyingi:

1 – Kwamba ni dhaifu na wameidhoofisha wahifadhi wakubwa wa Hadiyth. Ameidhoofisha al-Bayhaqiy na amenukuu kudhoofishwa kwake kutoka kwa Sufyaan ath-Thawriy, ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy, Ahmad bin Hanbal, ´Aliy bin al-Madiyniy, Yahyaa bin Ma´iyn na Muslim bin al-Hajjaaj. Hawa ni vigogo wa maimamu wa Hadiyth. Hata kama at-Tirmidhiy amesema kuwa Hadiyth ni ”nzuri na Swahiyh”, basi hawa wanatangulizwa mbele yake. Bali hata kama mmoja wao angekuwa peke yake, basi angelitangulizwa mbele ya at-Tirmidhiy kwa makubaliano ya watu wa elimu.

2 – Kwamba lau ingesihi, basi ingefasiriwa kuwa ni zile soksi ambazo mtu anaweza kutembea nazo. Namna hiyo ndio mtu anakusanya dalili. Katika Hadiyth hakuna ujumla unaoweza kushikiliwa.

3 – al-Bayhaqiy amesimulia kutoka kwa Abul-Waliyd an-Naysaabuuriy kwamba ameifasiri kuwa ni kupangusa juu ya soksi zilizo na viatu vilivyoshikamana, si soksi peke yake na kiatu peke yake. Basi ni kana kwamba alisema kwamba alipangusa juu ya soksi zake zilizo na viatu vilivyoshikamana.”

Ama maneno yake Imaam an-Nawawiy “Maswahiba zetu wametoa hoja kwamba haiwezekani kuendelea kutembea juu yake”, inaweza ikawa ni hoja kwa yule anayefuata kibubusa. Ama kwa mwanazuoni wa Hadiyth na misingi hoja kwake ni Qur-aan na Sunnah na yale yanayorejea kwayo katika dalili nyingine. Kanuni ya mjadala inaamuru kwamba hoja yenye nguvu ijibiwe kwa iliyo na nguvu zaidi, Hadiyth ijibiwe kwa mfano wake au kwa Aayah, si kwa maoni wala kwa kipimo. La sivyo itakuwa ni kwenda katika yale waliyosimangwa kwayo watu wa maono (أهل الرأي)[2]. Katika mlango huu hakuna Aayah inayorudisha Hadiyth hii wala hakuna Hadiyth inayoirudisha. Bali zipo zinazoisapoti kutoka Qur-aan na Sunnah, kama ilivyotangulia. Na hii ndiyo hoja inayojulikana katika misingi.

Ama maneno yake “Kwamba ni dhaifu na wameidhoofisha wahifadhi”, kisha akanukuu kudhoofishwa kwake kutoka kwa waliowataja, basi jibu lake ni lile tulilotanguliza kabla katika shubuha ya tatu, kwa kuikabili kwa kusahihishwa na wale walioisahihisha. Zaidi ya hayo msingi wa kudhoofishwa kwake ni dai la kuwa ni yenye hali isiyo ya kawaida. Tumebainisha kwamba hali isiyo ya kawaida si dosari ya kudhoofisha kwa ujumla. Bali yeyote aliyekuwa mwadilifu na mwenye kuhifadhi vizuri, basi kupwekeka kwake katika kusimulia huwa ni sahihi, khaswa na ilihali imeungwa mkono na yaliyoripotiwa kwa maana yake katika Hadiyth ya vitambaa vinayofunika miguu iliyotangulia na ikaongezewa nguvu na matendo ya Maswahabah kama itakavyokuja. Ndiyo maana Imaam at-Tirmidhiy aliisahihisha. Haifichiki kwamba wanaoidhoofisha, hata wakiwa wengi kiasi gani, hoja yao katika kudhoofisha ni ile hali isiyo ya kawaida, jambo ambalo tayari umeshalijua. Basi hapa si mahali pa kupima kwa wingi au uchache, bali ni mahali pa kuleta dalili, kuhoji na kupima kwa kanuni zinazokubalika. La sivyo wingi si miongoni mwa hoja na ushahidi unaojulikana. Ndiyo maana wanazuoni wa misingi wamesema katika mjadala wa Hadiyth ya mpokezi mmoja kwamba kwa sababu tu wanazuoni wengi wamefanya kazi kinyume na Hadiyth iliyopokelewa na mpokezi mmoja, hakuzuii uwajibu wa kuifanyia kazi, kwa sababu kitendo cha wengi si hoja. Wameeleza kwamba hoja ni maafikiano na kitendo cha wengi si maafikiano, kwa sababu maafikiano ni makubaliano ya wanazuoni wote wa ijtihadi wa ummah. Kinyume chake masimulizi ya mpokezi mmoja ni hoja kwa yenyewe.

[1] Kwa maana katika kuraddi yale maoni yanayojuzisha kupangusa juu ya soksi nyembamba.

[2] Kwa maana Hanafiyyah ambao husimulia baadhi ya Hadiyth kulingana na maoni yao wenyewe ili kuunga mkono maoni ya maimamu wao. Utapata mifano ya hili katika kitabu changu “Ahkaam-ul-Janaa-iz”. Siwatakasi wengine kutokana na kitendo hichohicho. Kama unavyowezekana kujionea mwenyewe wafuasi wa an-Nawawiy pale wanapopindisha maana Hadiyth hii Swahiyh. Mwandishi (Rahimahu Allaah) amefanya vyema kabisa katika kuwaraddi – Allaah amlipe thawabu!

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 34-37
  • Imechapishwa: 07/04/2026