Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewashuhudia watu wa Yemen imani na uelewa[1]. Hakika wayemeni ni watu wachache kuongea na wenye kubobea kielimu, lakini  walikuwa na elimu yenye manufaa ndani ya mioyo yao na hawazungumzi isipokuwa kwa kile kiwango kinachohitajika. Huu ndio uelewa wenyewe na elimu yenye manufaa. Elimu ambazo ni bora katika kuifasiri Qur-aan na Sunnah na uzungumziaji wa yaliyo ya halali na yaliyo haramu ni yale yaliyopokelewa kwa Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah kwenda mpaka kwa wale maiamu wa Uislamu wanaotambulika na wenye kuigwa ambao tumekwishatangulia kuwataja. Elimu bora ni kuyadhibiti yale yaliyosimuliwa kutoka kwao, kuyafahamu na kuyaelewa. Yale yaliyozungumziwa kwa kina baada yao mara nyingi hayana kheri yoyote, isipokuwa kama ni maelezo ya maneno yao. Kuhusu yale yanayokwenda kinyume na maneno yao, kwa kiasi kikubwa ni batili au yasiyokuwa na manufaa yoyote. Isitoshe maneno ya wa mwanzo hao waliotajwa ni yenye kutosheleza bali na ziada. Hakuna haki inayopatikana kwa vile vizazi vilivyokuja baada yao isipokuwa inapatikana katika maneno ya wale wa mwanzo, tena kwa kufupiza kabisa. Na wala hakuna batili yoyote inayopatikana kwa vile vizazi vilivyokuja baada yao isipokuwa katika maneno yao kutapatikana yanayobainisha ubatilifu wake. Hayo atayaona yule mwenye kufahamu na kuyazingatia. Kunapatikana katika maneno ya wale wa mwanzo maana zenye kugonga na mfumo madhubuti ambavyo vile vizazi vilivyokuja baada yao hawaongozwi kwavyo wala kuyazunguka. Yeyote ambaye hatochukua elimu kutoka katika maneno yao basi atapitwa na kheri yote. Aidha atatumbukia katika batili nyingi na kulazimika kutazama usahihi wa maneno ya wale waliokuja nyuma kwa msaada wa kujeruhi, kuadilisha na kasoro. Yule ambaye hana uwezo huo hawezi kuamini kile anachonakili na atachanganyikiwa na haki kutokamana na batili. Kama ambavo wale wachache wa elimu hawatoamini yale anayosimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa Salaf, kwa sababu ya kutokuwa na utambuzi wa yaliyo sahihi na ambayo ni dhaifu. Kutokana na ujinga wake anaweza kuzingatia yote kuwa batili kwa sababu ya kutokujua ambayo ni sahihi na ambayo si sahihi.

[1]al-Bukhaariy (8/98) na Muslim (1/71).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 66-68
  • Imechapishwa: 22/09/2021