96 – Tambua ya kwamba ndoa ya starehe na kumuoa mwanamke kwa lengo kumhalalishia mume wake aliyetangulia ni haramu mpaka siku ya Qiyaamah.

97 – Fahamu ya kwamba kizazi cha Haashim wana fadhilah zao kwa sababu ya udugu wao pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tambua fadhilah za Quraysh, waarabu na makabila mengine yote. Zitambue nafasi zao na haki zao katika Uislamu. Aliyeachwa huru na watu ni katika wao. Zijue haki za watu wengine katika Uislamu. Zitambue fadhilah za Wanusuraji na wasia wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu yao. Vivyo hivyo familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – usiisahau! Zitambue fadhilah na utukufu wao. Vilevile majirani wake Madiynah – zitambue fadhilah zao!

98 – Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba wanazuoni bado ni wenye kuendelea kuraddi ´Aqiydah ya Jahmiyyah mpaka ilipofika katika ukhalifah wa watu fulani. Hapa ndipo Ruwaybidhwah walipoanza kuzungumzia katika mambo yanayohusu jamii. Wakatukana masimulizi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakachukua vipimo na maoni. Wakawakafirisha wenye kwenda kinyume nao. Hivyo mjinga na mghalilikaji akajipenyeza katika maneno yao na akafanya hivo yule asiyekuwa na elimu mpaka wakakufuru pasi na kujua. Ummah ukaangamia kwa mitazamo mbalimbali, wakakufuru kwa mitazamo mbalimbali, wakaingia katika uzandiki kwa mitazamo mbalimbali, wakapotea kwa mitazamo mbalimbali na wakafarikiana na kuzua kwa mitazamo mbalimbali, isipokuwa yule aliyekuwa imara juu ya maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), maamrisho yake na maamrisho ya Maswahabah zake. Hakumtia makosani yeyote katika wao na hakulivuka jambo lao. Yaliyowatosheleza yakamtosheleza na yeye na wala akawa hakutamani isiyokuwa njia na madhehebu yao. Akajua kuwa wao ndio walikuwa wakifuata Uislamu na imani sahihi. Matokeo yake akawafuata katika dini yake na akastarehe. Anatambua kuwa dini ina maana ya kuwaigiliza Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

99 – Tambua kuwa yule mwenye kusema matamshi yake ya Qur-aan ni kiumbe, ni mzushi. Mwenye kunyamaza na asiseme kuwa ni kiumbe wala si kiumbe, ni Jahmiy. Hivi ndivyo alivyosema Ahmad bin Hanbal. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi baada yangu, basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi jihadharini na mambo ya kuzua, kwani hakika ni upotevu. Jilazimiesheni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Ziumeni kwa magego yenu.”[1]

100 – Tambua ya kuwa maangamivu ya Jahmiyyah yamejitokeza kwa sababu ya kumfikiria Mola (´Azza wa Jall) na matokeo yake wakaingiza “Kwa nini?” na “Vipi?”. Wakaacha masimulizi na wakaweka kipimo. Hivyo wakawa wameilinganisha dini na akili zao. Ndipo wakaleta ukafiri wa wazi usiojificha. Wakawakafirisha viumbe na wakawa ni wenye kutenzwa nguvu, ndipo wakaanza kuzungumza kwa ukanushaji.

[1] Abu Daawuud (4602), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 98-100
  • Imechapishwa: 22/12/2024