Katika maudhui haya watu wamegawanyika katika makundi mawili:

1 – Wanafalsafa na watu wa aina yao, ambao wako mbali na ujuzi wa Hadiyth na wanazuoni wake. Hawana elimu ya kupambanua baina ya Hadiyth Swahiyh na dhaifu. Licha ya kwamba Hadiyth ni zenye kutambulika na zenye uhakika kwa mujibu wa wanazuoni, wanatilia mashaka juu ya kusihi kwake au juu ya uhakika wake.

2 – Watu wanaojidai kuzifuata Hadiyth na kuzifanya kazi. Kila pale wanapoiona Hadiyth fulani iliyosimuliwa na mpokezi mwaminifu au kuiona Hadiyth ambayo cheni yake ya wapokezi inaonekana kuwa Swahiyh, basi wao wanataka kuifanya kuwa sawa na zile ambazo wanazuoni wamehakikisha juu ya kusihi kwake. Hata ikipingana na Hadiyth Swahiyh inayojulikana, basi wanajaribu kuitafsiri kwa namna isiyo sahihi au kuifanya kuwa ni dalili katika masuala ya kielimu, ingawa wanazuoni wa Hadiyth wanajua kuwa Hadiyth hiyo ina makosa.

Kama jinsi Hadiyth ina dalili zinazoonyesha ukweli wake, pengine hata inaweza kuhakikishwa, basi vivyo hivyo inayo pia dalili zinazoonyesha na kuthibitisha uwongo wake. Kwa mfano Hadiyth zinazobuniwa na waongo miongoni mwa watu wa Bid´ah na waliochupa mipaka katika mambo ya fadhilah, kama zile zinazohusiana na siku ya ´Aashuuraa na kwamba mtu anayeswali Rak´ah mbili basi hupata thawabu kama wa Mtume fulani. Kuna kiasi kikubwa cha mambo hayo katika tafsiri za Qur-aan. Mfano wake ni ile Hadiyth inayotaja fadhilah za kila Suurah na inapatikana katika tafsiri ya Qur-aan ath-Tha’labiy, al-Waahidiy na az-Zamakhshariy. Hadiyth hizi ni za kubini kwa maafikiano ya wanazuoni wote. Ni kweli kwamba kuhusu athl-Tha’labiy alikuwa ni mtu mwema na mwenye dini, hata hivyo alikuwa kama mkusanyaji kuni usiku wa giza ambaye anakusanya kila anachokipata ndani ya vitabu vya tafsiri za Qur-aan; sahihi, dhaifu au zilizobuniwa. al-Waahidiy alikuwa swahiba yake na alikuwa na ufahamu zaidi wa lugha ya kiarabu, lakini alikuwa mbali zaidi na usalama na kuwafuata Salaf. al-Baghawiy alifupisha tafsiri ya Qur-aan ya ath-Tha´labiy, lakini akaondoa zile Hadiyth zilizotungwa na maoni ya wazushi.

Hadiyth zilizobuniwa katika vitabu vya tafsiri ni nyingi, kama zile zenye masimulizi ya wazi kuhusu kusoma jina Allaah kwa sauti ya juu na Hadiyth ndefu ya ´Ali kuhusu kutoa swadaqah pete yake wakati wa anaswali; ambayo imetungwa kwa makubaliano ya wanazuoni wote. Vivyo hivyo kuhusu yale yaliyopokelewa kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ

”… na kila watu wana mwenye kuongoza.”[1]

Ya kwamba ni ´Aliy. Vivyo hivyo kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

لِنَجْعَلَهَا لَكُمْ تَذْكِرَةً وَتَعِيَهَا أُذُنٌ وَاعِيَةٌ

”… na ibakie ni ukumbusho kwenu katika sikio linalobakisha kumbukumbu.”[2]

Ya kwamba ni sikio lako, ee ´Aliy.

[1] 13:7

[2] 69:12

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 67-70
  • Imechapishwa: 02/04/2025