18. Hapa unakuwa mwenye kutawaliwa

Huu ndio muktadha wa hali ya mja, basi rehema ya Mola wake, Mshindi na Mwenye rehema kwake ikahitajika kwamba amsaidie kwa jeshi jingine na ampe msaada mwingine ili kupambana na jeshi hili linalotaka kuangamiza maisha yake. Basi akamtumia Mtume Wake, akamteremshia Kitabu Chake na akamuimarisha kwa Malaika mtukufu anayekabiliana na adui yake shaytwaan. Hivyo kila anapomwamrisha shaytwaan kwa jambo, basi Malaika humwamrisha kwa jambo la Mola wake na humweleza lililomo katika kumtii adui wake miongoni mwa maangamizi. Huyu humjia mara moja na huyu mara moja. Mnusurikaji ni yule aliyenusuriwa na Allaah (´Azza wa Jall), mlindwa ni yule aliyelindwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Akamfanyia badala ya nafsi yake inayoamrisha uovu na nafsi yenye utulivu. Basi ikiwa nafsi ya uovu inamwamrisha na uovu, basi nafsi yenye utulivu humkataza. Na ikiwa nafsi ya uovu inamkataza kufanya kheri, basi nafsi yenye utulivu humwamrisha kufanya hilo. Basi yeye humtii huyu mara na huyu mara nyingine. Yeye ni katika yule anayemtawala zaidi mwingine. Huenda mmoja wao akashindwa kabisa kwa udhalili kiasi cha kutoweza kusimama tena kabisa.

Akamfanyia badala ya matamanio yanayombeba kumtii shaytwaan na nafsi ya uovu, nuru na umaizi na akili vinavyomrudisha kutoka kwenda na matamanio. Basi kila anapotaka kwenda pamoja na matamanio, humwita akili, umaizi na nuru:

”Tahadhari! Tahadhari! Hakika kuna maangamizi na maharibiko mbele yako. Nawe ni mawindo ya wanyang’anyi na wakata njia ikiwa utafuata mwongozo huyu.”

Basi huenda yeye humtii mtoa nasaha mara na humwonyesha njia yake na nasaha yake. Huenda akaenda nyuma ya mwongozi wa matamanio mara nyingine, akamshambulia njiani, akamuibia mali yake na akamvua nguo zake kisha akamuuliza:

”Unajua umepatwa vipi na haya?”

La kushangaza ni kwamba anajua yamempata namna gani. Anatambua njia iliyompata ndani yake na kuchukuliwa humo, lakini anakataa isipokuwa kuifuata. Kwa sababu mwongozi wake ameshapata uwezo juu yake, akamtawala na akamzidi nguvu. Lau angalimdhoofisha kwa kwenda kinyume naye, kumkemea anapomwita na kupambana naye anapotaka kumshambulia, basi asingalimpata. Lakini yeye mwenyewe amempa uwezo juu ya nafsi yake na yeye ndiye aliyempa mkono wake, basi hali yake ni kama ya mtu anayempa adui yake mkono wake kisha adui huyo anamtesa kwa mateso mabaya naye analia kuomba msaada lakini hapati msaada wowote. Ndivyo anavyojisalimisha kwa shaytwaan, matamanio na nafsi yake inayoamrisha maovu, kisha anatafuta kuokoka lakini hawezi.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 04/08/2025