Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

138 – Tunaamini adhabu ya kaburi kwa yule mwenye kuiistahiki, maswali ya Munkar na Nakiyr ndani ya kaburi lake kuhusu Mola, dini na Mtume Wake, kutokana na vile ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum).

MAELEZO

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ametaja katika “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” ya kwamba siku ya Mwisho kunaingia ndani yake kila kinachotokea baada ya kifo; adhabu na neema za ndani ya kaburi, Kufufuliwa, Kufanyiwa hesabu, Mizani, kutawanywa kwa madaftari, Pepo na Moto –anayepinga kitu katika hayo basi anazingatiwa si mwenye kuamini siku ya Mwisho. Hatupekui siku ya Qiyaamah na mambo mengine yote yaliyofichikana yanayohusiana nayo. Tunategemea yaliyokuja ndani ya Qur-aan na Sunnah pasi na kupekua mambo hayo wala kuyazungumza pasi na dalili.

Kaburi ni kituo kati ya dunia na Aakhirah, kama ilivyo katika Aayah:

وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ

”Nyuma yao kuna kizuzi mpaka siku watakayofufuliwa.”[1]

Kaburi ni kituo cha kusubiri ambapo watu baadaye watapelekwa katika kufufuliwa na kufanyiwa hesabu. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ametaja kwamba kuna aina tatu za maisha:

1 – Maisha ya duniani ambapo ni mahali pa matendo na kuchuma.

2 – Maisha ya ndani ya kaburi ambayo ni maisha ya muda. Kwa ajili hiyo ni kosa kusema kaburi ni mapumziko yake ya mwisho.

3 – Maisha ya milele, ima Peponi au Motoni.

[1]23:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 193-194
  • Imechapishwa: 10/12/2024