17. Tunasimama pale iliposimama Qur-aan na Sunnah

86 – Yuunus bin ´Abdil-A´laa amesema:

”Nilimsikia Abu ´Abdillaah Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy (Radhiya Allaahu ´anh) akisema wakati alipoulizwa kuhusu sifa za Allaah na kile anachoamini: ”Allaah (Ta´ala) anayo majina na sifa yaliyotajwa ndani ya Kitabu Chake na ambayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaeleza ummah wake. Hakuna yeyote katika viumbe wa Allaah (Ta´ala) ambaye inafaa kuyarudisha. Kwa sababu Qur-aan imeyateremsha na yamesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia wapokezi wenye kuaminika. Yule anayepondoka kutokana nayo baada ya kumthibitikia hoja basi ni kafiri. Kabla ya hapo anapewa udhuru kutokana na ujinga kwa sababu ujuzi wa mambo hayo haufikiwi kwa akili, kuonekana wala kufikiria. Hatumtuhumu ukafiri yule ambaye ni mjinga kabla ya kusimamiwa na hoja.”

87 – Abu Bakr al-Humaydiy amesema:

”Miongoni mwa ´Aqiydah ni kuamini yale yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah, kama vile:

وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Mayahudi wakasema: “Mkono wa Allaah imefumbwa”. Mikono yao ndio iliyofumbwa na wamelaaniwa kwa yale waliyoyasema. Bali mikono Yake imekunjuliwa.”[1]

وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

“… na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.”[2]

Hatuzidishi juu yake na wala hatuzifasiri. Tunasimama pale iliposimama Qur-aan na Sunnah na kusema:

الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[3]

Atakayedai kinyume na haya ni mtu wa batili na Jahmiy.”[4]

al-Humaydiy alikuwa ni imamu mwenye kuhifadhi na mtukufu ambaye alichukua elimu kutoka kwa Sufyaan na ash-Shaafi´iy. Miongoni mwa ambao wamepokea kutoka kwake ni al-Bukhaariy katika ”as-Swahiyh al-Musnad”. Alikufa mwaka wa 219.

88 – Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam amesema:

”Hadiyth hizi ni Swahiyh. Wapokezi wenye kuaminika wamezifikisha hawa kutoka kwa hawa mpaka zikatufikia. Hapana shaka tunaamini kuwa ni haki. Lakini tukiulizwa ni vipi anaweka mguu Wake au anacheka namna gani, tunasema kuwa hatuzifasiri na wala hatukumsikia yeyote akizifasiri.”

Abu ´Ubayd alikuwa ni wa kipekee katika wakati wake. Imaam Ishaaq bin Raahuuyah amesema:

”Allaah anapenda uadilifu; Abu ´Ubayd ni mjuzi zaidi kuliko mimi, ash-Shaafi´iy na Ahmad bin Hanbal!”

89 – al-Khallaal amesema katika ”as-Sunnah” yake:

”al-Marwaziy ametuhadithia: ”Nilimuuliza Ahmad bin Hanbal kuhusu Hadiyth kuhusu sifa ambapo akajibu: ”Tunazipitisha kama zilivyokuja.”

90 – Imaam Ahmad amesema tena:

”Hatuvuki Qur-aan na Hadiyth. Tunasema yale Aliyoyasema, tunamsifu kama Alivyojisifu na hatuvuki hayo. Tunaamini yale yote yaliyomo ndani ya Qur-aan; ya wazi na yenye kutatiza. Haturudishi nyuma sifa yoyote kwa sababu ya matusi.”

91 – Abu ´Iysaa at-Tirmidhiy amesema katika ”al-Jaamiy´” yake ambacho ni moja katika vile vitabu vitano vya Kiislamu:

”Wanazuoni wengi wamesema kuhusu Hadiyth hii na mapokezi mfano wake kuhusu sifa za Allaah na kushuka kwa Mola (Tabaarak wa Ta´ala) kila usiku katika mbingu ya chini kwamba ni Swahiyh. Mtu anatakiwa kuziamini pasi na kuzifikiria wala kuziulizia namna. Haya yamepokelewa kutoka kwa Maalik bin Anas, Sufyaan bin ´Uyaynah na ´Abdullaah bin al-Mubaarak ambao wamesema:

”Zipitisheni Hadiyth hizi pasi na kuzifanyia namna.”

Haya yamesemwa na wanazuoni wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Kuhusu Jahmiyyah yameyapinga mapokezi haya na wakasema kuwa kufanya hivo ni kufananisha. Allaah mara nyingi ndani ya Kitabu Chake ametaja mkono, kuona na kusikia. Jahmiyyah wakafasiri kinyume na vile walivyofasiri wanazuoni na wakasema:

”Allaah hakumuumba Aadam kwa mkono Wake. Maana yake ni neema.”[5]

Ibn Raahuuyah amesema:

”Hakika hapana vyenginevyo ni kufananisha pale atakaposema mkono ni kama mkono wangu, kusikia ni kama kusikia kwangu. Huku ndio kufananisha. Lakini akisema kama alivosema Allaah, kuwa ”mkono”, ”usikizi” na ”uoni”, pasi na kuzifanyia namna wala kuamini kuwa mkono inafanana na mikono mingine au ni kama mikono mingine. Huku sio kufananisha. Ni kama alivosema Allaah (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[6][7]

[1] 05:64

[2] 39:67

[3] 20:5

[4] Usuwl-us-Sunnah, uk. 88-91

[5] al-Jaamiy´ (662).

[6] 42:11

[7] al-Jaamiy´ (662).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 84-87
  • Imechapishwa: 04/06/2024