77 – ´Amr bin Muhammad bin al-Hasan ametukhabarisha: Baba yangu ametukhabarisha: Sulaymaan bin al-Mughiyrah ametuhadithia, kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Anas:

”Wakati ilipomalizika eda ya Zaynab, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: ”Ee Zayd, hakuna mtu ninayemwamini zaidi kama wewe. Hakuna mtu ambaye nina imani kwake kama wewe. Hivyo basi niachie naye huru.” Nikaondoka na kumkuta akioka unga wake. Mara tu nilipomuona, heshima yangu kwake ilipanda sana kiasi cha kwamba sikuweza kustahimili kumtazama, kwa sababu nimejua kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekwishamposa. Nikamgeuzia mgongo na kusema: “Ee Zaynab, pata bishara njema! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amenitumia kwako; anakuposa.” Akasema: ”Sifanyi chochote kabla ya amri ya Mola wangu.” Akaenda sehemu yake ya kuswalia ambapo              Qur-aan ikateremshwa. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingia kwake pasi na kuomba idhini.”[1]

78 – ´Aliy bin Hujr ametukhabarisha, kutoka kwa Ismaa´iyl, kutoka kwa ´Abdullaah bin Diynaar, kutoka kwa Ibn ´Umar, ambaye ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituma kikosi na akamteua Usaamah bin Zayd kuwa kiongozi wake, ambapo baadhi ya watu wakasema vibaya uongozi wake. Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ikiwa mnasema vibaya uongozi wake, basi hapo kabla mlikuwa mkisema vibaya uongozi wa baba yake. Naapa kwa Allaah! Alikuwa anastahiki kwa uongozi na alikuwa ni miongoni mwa watu wanaopendeza zaidi kwangu. Baada yake huyu pia ni miongoni mwa watu wanaopendeza zaidi kwangu.”[2]

79 – Ahmad bin Sulaymaan ametukhabarisha: Muhammad bin ´Ubayd ametukhabarisha: Waa-il bin Daawuud ametukhabarisha: Nimemsikia al-Bahiy akisimulia kutoka kwa ´Aaishah aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kamwe hakupeleka kikosi isipokuwa alimteua Zayd bin al-Haarithah kuwa kiongozi wake. Kama angeendelea kuishi baada yake, angalimteua kuwa kiongozi wake.”

[1] Muslim (1428).

[2] al-Bukhaariy (4250) na Muslim (2426).

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 09/09/2026