´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 17: Bid´ah ni kitu gani na ni vyepi vigawanyo vyake?

Jibu: Bid´ah ni kwenda kinyume na Sunnah. Imegawanyika aina mbili:

1 – Bid´ah ya kiitikadi. Ni kuwa na I´tiqaad kinyume na yale aliyoelezea Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imetajwa katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ni ipi hiyo, Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litalofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu”[1]

Ambaye yuko katika wasifu kama huu basi anafuata Sunnah safi. Anayefuata mapote mengine ni mzushi. Kila Bid´ah ni upotevu na zinatofautiana kwa kiasi na zilivyo mbali na Sunnah.

2 – Bid´ah ya kimatendo. Ni kule kuabudu kwa njia ambayo haikuweka Allaah wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kuharamisha kitu ambacho Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamehalalisha. Hivyo yule mwenye kuabudu kwa njia ambayo haikuwekwa katika Shari´ah au akaharamisha kitu ambacho dini haikuharamisha, ni mzushi.

MALEZO

Maana ya Bid´ah kilugha ni kwenda kinyume na Sunnah. Maana yake ya kidini ni kila imani au kitendo ambacho hakikusuniwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtunzi wa kitabu amezigawanya Bid´ah mafungu mawili:

1 – Bid´ah ya kiitikadi.

2 – Bid´ah ya kimatendo.

Bid´ah ya kiitikadi ni mbaya zaidi kuliko Bid´ah ya kimatendo. Mfano wa Bid´ah ya kiitikadi ni:

1 – Bid´ah ya Jahmiyyah katika kupinga majina na sifa za Allaah.

2 – Bid´ah ya Mu´tazilah ya kupinga majina na Qadar ya Allaah, nadharia yao ya kuamini kwao kwamba Qur-aan imeumbwa na kukanusha kwao kuonekana kwa Allaah Aakhirah.

3 – Bid´ah ya Murji-ah ambao wanadai kuwa mtenda dhambi kubwa ni muumini mwenye imani kamilifu.

4 – Bid´ah ya Shiy´ah waliopindukia ambao wanawanyanyua watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ngazi zaidi ya walizopewa na Allaah (´Azza wa Jall). Sambamba na hilo wanawapuuza Maswahabah wengine wote.

5 – Bid´ah ya Ashaa´irah wambao wanazipindisha sifa za Allaah (´Azza wa Jall).

Zote hizi ni Bid´ah za kiitikadi na zinatofautiana. Baadhi katika hizo ni kufuru, kama mfano wa mwenye kuitakidi kuwa Qur-aan imeumbwa. Baadhi yake ni chini ya hapo licha ya kuwa zinazingatiwa kuwa ni Bid´ah zenye madhambi mazito. Nazo pia zinatofautiana; baadhi ni khatari zaidi na ziko mbali zaidi na haki. Kadhalika Bid´ah ya Taswawwuf iliyoanza kwa aina fulani ya kuyapa nyongo mambo ya kidunia na baadaye ikapea katika kiwango cha kufuru, kama mfano wa imani ya kusema kwamba kila kiumbe ni Allaah na kwamba Allaah amekita katika kila kiumbe. Zote hizi ni Bid´ah za kiitikadi.

Kuhusu Bid´ah za kimatendo nazo pia zimegawanyika sampuli mbili:

1 – Bid´ah ya kimatendo iliyozuliwa na inayopingana na Shari´ah. Kama mfano wa ´ibaadah za Suufiyyah kwa nyimbo, kucheza,  densi na mfano wa hayo.

2 – Bid´ah ya kuongeza ambayo ni kuongeza juu ya kitu ambacho msingi wake umewekwa katika Shari´ah. Mzushi huyu anaongeza sifa fulani juu ya kitu kile kilichosuniwa. Kwa mfano imewekwa katika Shari´ah na Sunnah kufanya Tasbiyh, Tahmiyd, Takbiyr na Tahliyl baada ya swalah.  Lakini kuyafanya hayo kwa njia na  mtindo wa pamoja ni jambo lililoongezwa. Mfano wa jambo hilo lilifanyika na waswaliji katika msikiti wa Kuufah ambapo ´Abdullaah bin Mas´uud akawakaripia.

Mfano mwingine wa jambo hilo ni yale yanayosemwa na baadhi ya Hizbiyyuun ambapo wanakubaliana wote kufunga siku fulani na kufutari wote kwa pamoja nyumbani kwa fulani.

Vivyo hivyo baadhi ya watu huongeza kitu ambacho hakikuwekwa katika Shari´ah juu ya kitu kilichowekwa katika Shari´ah kwa sababu kuna mtu wa hapo kale ambaye amekionelea kuwa ni kizuri au kwa ajili ya kuwafuata kichwa mchunga wengine. Yote haya ni katika Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[2]

 “Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[3]

Mzushi ni mwenye kuikosoa Shari´ah ni kama kwamba Allaah anasema kuwa yeye amejua kitu ambacho hakikujulikana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yeyote atakayezusha uzushi na akadai kuwa ni mzuri, basi amemtuhumu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufanya khiyana.”[4]

Kwa hiyo ni lazima kutahadhari kutokamana na Bid´ah aina zote, kubwa na ndogo, za kiitikadi na za kimatendo. Kitu bora ambacho mtu anaweza kufikia katika maisha yake ni kuishi kwa mujibu wa Sunnah ili aweze kusalimika kutokamana na adhabu baada ya kufa.

Tunapaswa kujua kwamba Bid´ah ni yale yaliyozuliwa yanayohusiana na dini. Kuhusu mambo yaliyozuliwa ya kidunia hayaingii ndani ya sampuli hiyo.

[1] at-Tirmidhiy (2641) na al-Haakim (1/128).

[2] al-Bukhaariy (2697).

[3] Muslim (1718).

[4] al-I´tiswaam (1/297) ya ash-Shaatwibiy.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 94-97
  • Imechapishwa: 21/10/2021